Mahakama yalifunga shirika la haki za binadamu Urusi
28 Desemba 2021Hatua ya kufungwa kwa shirika hilo, inahitimisha mwaka mmoja wa ukandamizaji dhidi ya harakati za wapinzani na mashirika ya kutetea haki za binadamu.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Memorial lililoamriwa kufungwa hii leo na mahakama ya juu ya Urusi lilianzishwa mwishoni mwa miaka ya utawala wa Umoja wa Kisovieti ambapo lilijikita zaidi katika kuhifadhi kumbukumbu za uhalifu uliofanywa enzi za utawala wa Stallin. Shirika hilo hivi karibuni, limekuwa likipaza sauti zaidi dhidi ya ukandamizaji wa wakosoaji chini ya utawala wa sasa wa Rais Vladmir Putin.
Akisoma hukumu hii leo, Jaji Alla Nazarova aliamuru kufungwa kwa shirika la Memorial International, muundo mzima wa shirika hilo na matawi yake ya kieneo kwa kushindwa kuyapa utambulisho mashapisho yake kama taasisi ya kigeni na hivyo kukiuka sheria
Urusi imesema inachokifanya ni kutekeleza sheria za kukabiliana na misimamo mikali na kuilinda nchi dhidi ya ushawishi wa mataifa ya kigeni. Shirika la habari la Interfax mapema leo liliripoti likimnukuu mwanasheria wa shirika la kutetea haki za binadamu la Memorial kuwa kesi hiyo ilikuwa na msukumo wa kisiasa na watakata rufaa katika mahakama ya Urusi na mahakama ya Ulaya ya haki za binadamu.
Akizungumzia hatua ya leo ya mahakama, mmoja wa wajumbe wa bodi ya shirika hilo Oleg Orlov amesema kuwa Memorial ni shirika maalumu lenye itikadi ya kipekee lenye mchanganyiko wa kile kinachoitwa shughuli husika za kutetea haki za binadamu pamoja na tafiri za kihistoria na kufahamu Urusi ilikopita kihistoria katika karne ya 20.
Vikwazo vya kisheria vilianza 2015
Mamlaka za Urusi zililiweka shirika la kutetea haki za binadamu la Memorial katika orodha rasmi ya taasisi za kigeni mnamo mwaka 2015, hatua iliyohusisha vikwazo kadhaa katika kuendesha shughuli zake.
Mwezi uliopita, waendesha mashtaka walilituhumu kituo cha shirika hilo cha chenye makao yake mjini Moscow na shirika mama la Memorial international kwa muundo wake unaokiuka sheria ya taasisi za kigeni na wakaitaka mahakama kulifunga.
Akizungumza mwishoni mwa kesi hiyo leo, mwendesha mashtaka wa serikali alisema, shirika hilo la kutetea haki za binadamu liliratibu kampeni kubwa za vyombo vya habari zilizokuwa zimekusudia kudharau mamlaka za Urusi.