1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya Mali yamtangaza Goita rais wa mpito

29 Mei 2021

Mahakama ya Katiba ya Mali imemtangaza Kanali Assimi Goita kuwa rais mpya wa mpito kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Rais Bah Ndaw ambaye amejiuzulu.

https://p.dw.com/p/3u97A
Mali Oberst Assimi Goita, neuer Übergangspräsident
Picha: AP Photo/picture alliance

Katika uamuzi wake mahakama hiyo imesema Goita aliyeongoza mapinduzi ya kijeshi siku ya Jumatatu anapaswa kujaza nafasi hiyo. Uamuzi huo unazidisha mkwamo ambapo viongozi wa mataifa ya Afrika Magharibi wakiwa wanajiandaa kukutana siku ya Jumapili kuzungumzia hatua ya kukabidhi madaraka, ambayo inahatarisha harakati za kuelekea kwenye demokrasia na kudhoofisha mapambano dhidi ya wapiganaji wa jihadi katika ukanda huo.

Goita alikuwa makamu wa rais baada ya kuongoza mapinduzi mwezi Agosti mwaka uliopita na kumuondoa madarakani Rais Ibrahim Boubacar Keita. Ndaw na Waziri Mkuu, Moctar Ouane ambao walishikiliwa baada ya mapinduzi hayo walijiuzulu siku ya Jumatano,wakiwa bado kizuizini. Viongozi hao waliokuwa katika serikali ya mpito waliachiwa huru siku ya Alhamisi. Hayo ni mapinduzi ya pili kufanyika Mali ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Mali | Interimspräsident Bah Ndaw
Bah Ndaw alijiuzulu siku ya Jumatano kama rais wa mpitoPicha: Amadou Keita/Reuters

Kanali Goita ambaye aliwashutumu Ndaw na Ouane kwa kukiuka hati ya makubaliano kuhusu serikali ya mpito na kushindwa kuwasiliana naye kuhusu kufanya mabadiliko ya baraza la mawaziri, ambapo maafisa wawili wa kijeshi walipoteza nafasi zao. Kiongozi huyo wa kijeshi pia aliwashutumu Ndaw na Ouane kwa kushindwa kuituliza hali ya mambo nchini Mali, ukiwemo mgomo wa wiki iliyopita ulioandaliwa na shirikisho la vyama vya wafanyakazi.

Goita: Hatukuwa na njia nyingine

Siku ya Ijumaa, Goita alisema hawakuwa na njia nyingine ispokuwa kuingilia kati. ''Tulilazimika kuchagua kati ya machafuko na mshikamano ndani ya vikosi vya ulinzi na usalama na tulichagua kushikamana,'' alifafanua Goita.

Kanali huyo wa jeshi amesema atamchagua waziri mkuu ndani ya siku chache zijazo. Matamshi hayo aliyatoa Ijumaa usiku. Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu achukue madaraka, Goita ameyasema hayo baada ya kufanya mazungumzo na viongozi wa kisiasa na vyama vya kiraia mjini Bamako.

Kanali Goita amesema waziri mkuu atatoka miongoni mwa wajumbe wa muungano wa upinzani M5-RFP, ulioongoza maadanamano dhidi ya Keita mwaka jana. Jeamille Bitar, mwanachama wa muungano huo amesema mtu wanayempendekeza kushika nafasi hiyo ni Choguel Maiga, aliyekuwa waziri katika serikali iliyopita.

Weltspiegel | Bamako, Mali | Militärputsch, Protest gegen Frankreich
Baadhi ya waandamanaji wa Mali wakipeperusha bendera za Mali na UrusiPicha: Michele Cattani/AFP

Mapema siku ya Ijumaa mamia ya wananchi wa Mali waliandamana katika mji mkuu wa Bamako kuliunga mkono jeshi pamoja na Urusi. Baadhi ya waandamanaji walikuwa wakipeperusha bendera za Urusi na kubeba mabango yanayoishutumu Ufaransa, wakiitaka nchi hiyo iondoke Mali.

Urusi yapongeza

Wakati huo huo, Urusi imepongeza hatua ya jeshi la Mali kuwaachia viongozi wa mpito, ikisema nchi hiyo inaelekea katika njia sahihi na imetoa wito wa kufanyika mazungumzo kati ya wadau wote wa kisiasa. Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema kuwa mazungumzo hayo yatasaidia kupatikana kupatikana kwa umoja na utulivu.

Urusi imesema inaifuatilia kwa ukaribu matukio yanayoendelea nchini Mali. Urusi imewatolea wito viongozi wa sasa kurejesha ushirikiano na Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS na pia imeihimiza Mali kuandaa uchaguzi wa kidemokrasia.

(AFP, Reuters)