Mahakama ya kijeshi Uganda yawatia hatiani wapinzani 16
22 Oktoba 2024Upande wa mashtaka umedai kuwa wanachama 16 wa Jukwaa la Umoja wa Kitaifa, pamoja na wengine ambao bado hawajakamatwa, walikutwa na vilipuzi kati ya Novemba mwaka 2020 na Mei 2021, wakati uchaguzi ulikuwa ukiendelea. Kwa mujibu wakili wa upande wa utetezi Shamim Malende amesema kesi hiyo ilikuwa na mashaka kwa jinsi ilivyosikilizwa ambapo baadaye watuhumiwa walikubali makosa ambayo awali waliyakana. Mwimbaji wa zamani na kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, amedai kuwa watu hao wamelazimishwa kukiri makosa yao na kuomba msamaha wa rais. Waandishi wa habari hata hivyo hawakuruhusiwa kuhudhuria kikao hicho. Vijana hao 16 wamekaa gerezani kwa miaka minne, na watafikishwa mahakamani hapo kesho ili kusomewa rasmi hukumu yao.