Mahakama ya katiba Kongo yathibitisha ushindi wa Tshisekedi
10 Januari 2024Mahakama ya katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imethibitisha kuchaguliwa tena kwa rais Felix Tshisekedi baada ya kukataa mashauri mawili ya kisheria yaliyowasilishwa kuyapinga matokeo yaliyozozaniwa ya uchaguzi wa mwezi uliopita.
Mahakama hiyo imemtangaza rasmi Tshisekedi kama mshindi wa uchaguzi huo. Uamuzi huo wa mahakama unamfungulia mlango Tshisekedi kuhudumu kwa awamu nyingine ya miaka mitano katika taifa hilo la pili kwa ukubwa barani Afrika.
Soma pia: Umoja wa Mataifa waonya kukithiri kwa matamshi ya chuki DRC
Mahakama ya katiba imethibitisha ushindi wa Tshisekedi licha ya ripoti za waangalizi huru wa uchaguzi kudai kulikuwa na mapungufu wakati na baada ya uchaguzi wa mwezi Desemba mwaka uliopita ambayo yaliwafanya wagombea wa upinzani kutaka uchaguzi urudiwe na kudai kulitokea wizi.