Mahakama ya Juu Marekani yabatilisha haki ya kutoa mimba
25 Juni 2022Siku ya Ijumaa, mahakama ya juu zaidi Marekani ilitoa uamuzi wake kwenye kesi iliyofuatiliwa kwa makini na wengi ya uavyaji mimba. Mahakama hiyo ilibatilisha haki ya wanawake kutoa mimba Marekani.
Rais wa Marekani Joe Biden amekosoa vikali uamuzi huo akisema ni ‘kosa la kusikitisha lenye athari kubwa'. Badala yake amehimiza maandamano ya amani miongoni mwa wanaoulaani na kuupinga uamuzi huo, huku akiyarai majimbo kuweka sheria zitakazoruhusu utoaji mimba.
Uamuzi huo umejiri baada ya waraka wa mahakama hiyo wa uavyaji mimba kuvujishwakwa vyombo vya habari vya Marekani mapema mwezi Mei.
Rasimu hiyo ilionesha kuwa Mahakama ya Juu ya Marekani ilikuwa tayari kutengua uamuzi huo wa kihistoria wa Roe v. Wade uliopitishwa mwaka 1973 na ambao uliweka haki ya kutoa mimba.
Nusu ya majimbo yatarajiwa kuweka vikwazo dhidi ya utoaji mimba
Uamuzi huo unawacha njia wazi kwa uwezekano wa majimbo nchini Marekani kupiga utoaji mimba marufuku.
Saa chache tu baada ya uamuzi huo wenye mtikisiko kutolewa, jimbo la Missouri, lilipiga marufuku utoaji mimba isipokuwa tu kama mimba ilitokana na kisa cha ubakaji au ngono kati ya marahimu- ndugu wa karibu.
Wanaotoa mimba Kenya wakumbwa na hofu
Jimbo la Dakota linatarajiwa kufuata mkondo huo. Gavana wake Kristi Noem ametoa tarifa akisema uavyaji mimba ni kinyume chas heria katika jimbo lake, ila tu kama sababu maalum ya kiafya au kimatibabu kuthibisha haja ya mja mzito kuharibu mimba.
Takriban nusu ya majimbo yote ya Marekani yanatarajiwa kupiga marufuku utoaji mimba. Yakiwa na matarajio kwamba uamuzi wa Roe v. Wade utabatilishwa, tayari majimbo 13 yalikuwa yameandaa miswada ya kisheria kwa lengo la kuharamisha kitendo hicho.
Mahakama ilisema nini?
Mahakama hiyo imesema ni wajibu wa kila jimbo kuamua kama litaruhusu uavyaji mimba au la. "Katiba hajaruhusu haki ya kutoa mimba; uamuzi wa Roe na Casey umebatilishwa na mamlaka ya kusimamia na kudhibiti uavyaji mimba unarudishwa kwa wananchi na wawakilishi wao waliochaguliwa,” mahakama ilisema hayo ikirejelea uamuzi wa mwaka 1992 wa uzazi wa mpango dhidi ya Casey ulioruhusu haki ya utoaji mimba.
Uvujishwaji wa rasimu ya mtizamo wa mahakama ya Juu kutoka kwa jaji Samuel Alito, ulisababisha maandamano ya nchi nzima, ikiwemo nje ya makaazi ya baadhi ya majaji wahafidhina wa mahakama hiyo.
Uamuzi wa Alito uliungwa mkono na majaji wengine wanne ambao ni wahafidhina: Clarence Thomas, Neil Gorsuch, Brett Kavanagh na Amy Coney Barrett.
Uamuzi huo umeshutumiwa na mashirika mbalimbali kimataifa likiwemo shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya afya ya uzazi na ngono, Amnesty International na Human Rights Watch.
(AFPE, DW)