1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiRwanda

Mahakama yamhukumu Munyemana kifungo cha miaka 24 jela

20 Desemba 2023

Aliyekuwa daktari raia wa Rwanda Sosthene Munyemana amehukumiwa kifungo cha miaka 24 jela na mahakama ya Ufaransa kwa kuhusika na mauaji ya kimbari ya watu wa jamii ya Watutsi mnamo mwaka 1994.

https://p.dw.com/p/4aMt8
Majina ya watu waliochinjwa walipokuwa wakikimbilia hifadhi kanisani nchini Rwanda mwaka 1994
Majina ya watu waliochinjwa walipokuwa wakikimbilia hifadhi kanisani nchini Rwanda mwaka 1994Picha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Mtaalamu huyo wa magonjwa ya wanawake na uzazi mwenye umri wa miaka 68 alikutwa na hatia ya mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya ubinadamu na kula njama ya kuandaa uhalifu wote huo.

Mawakili wake wamesema wanapanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Mwendesha mashtaka wa umma alikuwa anataka Munyemana ahukumiwe kifungo cha miaka 30 jela, kwa hoja kwamba vitendo vyake vimedhihirisha "tabia za mtu aliyefanya mauaji ya kimbari."

Kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa katika mahakama ya Assize katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris imetokea karibu miongo mitatu baada ya malalamiko kuwasilishwa dhidi ya daktari huyo wa zamani katika mji wa kusini magharibi mwa Ufaransa wa Bordeaux mnamo mwaka 1995.