Mahakama Ufaransa kutoa hukumu dhidi ya Kabuga
27 Mei 2020Felicien Kabuga mwenye umri wa miaka 84, anatuhumiwa kwa makosa saba ,yakiwemo uchochezi wa mauwaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya ubinadamu. Mahakama ya kimataifa kwa ajili ya Rwanda,iliotowa waranti wa kukamatwa kwake tangia mwaka 1997, imesema kwamba Kabuga ni miongoni mwa vigogo tisa wanaotafutwa kwa kuhusika na mauwaji ya kimbari ya watu laki nane wa kabila la Watutsi na wahutu waliowasaidia.
Alikamatwa na polisi mjini Paris mapema mwezi huu, baada ya kuukwepa mkono wa sheria kwa zaidi ya miaka 26.
Kwa mujibu wa mashitaka ya mahakama ya kimataifa kwa ajili ya Rwanda (ICTR) ni kwamba Kabuga alimiliki Radio Television des Mille Collines (RTLM) na kuitumia kwa ajili ya uchochezi wa chuki za kibakila baina ya Wahutu na Watutsi.
Kabuga anatuhimiwa pia kuunda na kufadhili pamoja na wengine, kundi la wanamgambo wa kikabila ambao walitekeleza mauwaji hayo ya kimbari. Mahakama ya rufaa ya jijini Paris itaamua ama kumkabidhi Kabuga kwa mahakama maalum ya kimataifa ambayo ilichukuwa nafasi ya ile ilokuwa inashughulikia kesi za mauwaji ya kimbari nchini Rwanda iliyokuwa mjini Arusha nchini Tanzania au kuruhusiwa achiliwe kwa dhamana kufuatia ombi la mawakili wake.
Waendesha mashtaka wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wametoa ombi la kutaka Kabuga apelekwe katika vizuizi vya Umoja wa Mataifa, mjini The Hague,Uholanzi na kesi yake iendeshwe na mahakama hiyo.
Toka mwaka 2012 ,mahakama hiyo maalum ilichukuwa nafasi ya chombo cha Umoja wa Mataifa cha kushughulikia kesi za washukiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 ambacho kiliwahukumu washukiwa 62 miongoni mwao 14 walikutwa bila hatia, mnamo kipindi cha miaka 17 ya kazi ya mahakama hiyo mjini Arusha.
Kwa mujibu wa jalada la mwendesha mashataka wa jiji la Paris, mnamo kipindi hicho cha miaka 26, Kabuga aliishi katika nchi kadhaa zikiwemo Ujerumani,Ubeljiji, DRC, Kenya na Uswisi, kabla ya kukamatwa kwenye viunga vya mji mkuu wa Ufaransa, Paris.