Lula anaweza kufungwa wakati akisubiri rufaa yake
5 Aprili 2018Lula alikuwa na matumaini ya kukaa uraiani wakati mchakato wa kusikilizwa rufaa yake ukiwa unaendelea. Uamuzi huo umefikiwa mapema leo baada ya majaji wa Mahakama ya Juu ya Brazil waliokuwa wakisikiliza shauri hilo kujadiliana kwa muda wa saa 10 na hatimaye majaji sita kati ya 11 wa mahakama hiyo kulipinga ombi hilo, huku majaji watano wakiliunga mkono.
Akizungumza baada ya kura kupigwa, Rais wa mahakama hiyo, Carmen Lucia aliyepiga kura ya mwisho ya kulikataa ombi la Lula na kuzima ndoto za mwanasiasa huyo, amesema kuahirisha hukumu ya Lula, kunaweza kusababisha akapata kinga ya kutoshtakiwa.
''Kulingana na kura tulizopiga, Mahakama ya Juu inalikataa ombi hilo, na tumewashinda jaji Gilmar Mendes, Dias Toffoli, Ricardo Lewandowski, Marco Aurelio na Celso de Mello waliokuwa wanaunga mkono kuahirishwa kwa hukumu hiyo. Katiba inalinda haki ya kila raia ambayo ndio msingi wa demokrasia, lakini pia inahakikisha sheria ya makosa ya jinai inatumika,'' alisema Lucia.
Uamuzi huo wa mahakama unamaanisha kuwa Lula mwenye umri wa miaka 72, huenda akaanza kutumikia kifungo chake cha miaka 12 gerezani hivi karibuni. Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa rais huyo wa zamani wa Brazil tayari anaweza kufungwa leo. Kutokana na umaarufu wake, Lula alikuwa anapewa nafasi kubwa ya kushinda katika uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mwezi Oktoba, iwapo angeshiriki.
Hata hivyo uamuzi wa mahakama huenda ukahitimisha harakati zake za kisiasa. Mawakili wa Lula wamesema mteja wao ana haki ya kikatiba ya kuwa nje ya magereza hadi hapo rufaa yake itakapokamilika.
Alihukumiwa mwaka uliopita
Mwaka uliopita, Lula aliyekuwa rais wa Brazil kuanzia mwaka 2003 hadi 2010, alihukumiwa kifungo cha miaka 12 na mwezi mmoja gerezani, baada ya kukutwa na hatia ya kupokea rushwa kutoka kwenye kampuni kubwa ya ujenzi, ili iweze kushinda zabuni za serikali na kupatiwa mikataba. Lula anakabiliwa pia na mashtaka mengine ya kutakatisha fedha pamoja na kuingilia shughuli za mahakama.
Zaidi ya majaji na waendesha mashtaka 5,000 waliwasilisha katika Mahakama ya Juu ombi la kutaka Lula afungwe jela haraka iwezekanavyo. Majaji pia walipokea maelfu ya baruapepe zinazotoa ombi kama hilo.
Lula alikutwa na hatia hiyo baada ya uchunguzi wa muda mrefu unaojulikana kama ''Operation Car wash'' katika kashfa hiyo ya rushwa. Rais wa Brazil Michel Temer na rais wa zamani Dilma Rousseff wamehusishwa pia katika uchunguzi huo ambao unaendelea kuzitikisa siasa za Brazil.
Kesi ya Lula imewagawa Wabrazil ambao wameandamana kwenye miji mbalimbali, huku katika mji wa Sao Paulo wakitaka kiongozi huyo afungwe gerezani na kuzuiwa kushiriki katika uchaguzi wa Oktoba. Waandamanaji kwenye miji mingine ikiwemo Brasilia wanataka Lula aachiwe huru, wakisema kuwa kesi yake imeendeshwa kisiasa.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, DPA
Mhariri: Bruce Amani