Mahakama Afrika Kusini yalitaka bunge kumuwajibisha Zuma
29 Desemba 2017Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini, imetoa uamuzi huo leo na kusema kuwa bunge lilishindwa kumwajibisha Rais Jacob Zuma kutokana na kashfa ya kutumia fedha za umma, kukarabati makazi yake binafsi, ya Nkandla. Hivyo mahakama imetaka bunge kuanza mchakato wa kumtoa madarakani kiongozi huyo.
Uamuzi huo ni pigo la mwisho la kimahakama, katika kashfa inayomkabili Zuma, ambaye pia anakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa umma akitakiwa kujiuzuliu wadhifa wake katika nchi hiyo iliyo na neema ya uchumi wa viwanda, kabla ya uchaguzi wa 2019. Hata hivyo haikuwekwa wazi mara moja ni hatua gani bunge litachukua.
Akitoa uamuzi huo leo, Jaji Chris Jafta alisema wamejiridhisha kuwa bunge halikutimiza wajibu wake. Uamuzi huo uliungwa mkono na wengi mahakamani hapo na ulionyeshwa mubashara katika luninga.
"Kwa mtazamo wetu, mchakato wa suala hilo haukuendana na kifungu cha 89. Bunge lilijadili na kuchagua kupiga kura ya kutokuwa na imani.-halikujiridhisha kuwa uvunjwaji wa katiba, katika suala hilo, ulikuwa umejikita katika kutafakari kifungu hicho. Hivyo basi, tunahitimisha kuwa bunge halikuweza kumwajibisha rais kutokana na makosa yake kama inavyotakiwa katika kifungu cha 89,``alisema
Jafta alisema imeelezwa vyema, katika kifungu cha 89 kinachodokeza wajibu wa bunge kutunga sheria hasa zile za kumuondoa rais madarakani. Akaongeza kuwa kwa kushindwa kujumuisha sheria hizo, bunge limeshindwa kutimiza wajibu wake.
Chama cha mrengo wa kushoto cha Economic Freedom Fighter, na vyama vidogo vya upinzani, ndivyo vilivyopeleka suala hilo katika mahakama ya katiba.
Zuma, yupo katika nafasi mbaya kwa sasa, baada ya makamu wa rais Cyril Ramaphosa, kupata ushindi mwembamba na kupata nafasi ya kukiongoza chama tawala cha Zuma, ANC wiki iliyopita. Hata hivyo bado Zuma ana nafasi muhimu katika chama hicho na tayari alishapenya katika kura za kutokuwa na imani naye.
Wakati huo huo, ANC imetoa taarifa na kusema kuwa kitapitia uamuzi huo na kujadili madhara yake katika kikao cha Kamati kuu ya chama hicho, kitakachofanyika, Januari 10, 2018.
Tangu Ramaphosa achaguliwe, randi ya Afrika Kusini imekuwa dhabiti katika siku za mwisho za mwaka. Imepanda kwa zaidi ya asilimia 10 dhidi ya dola.
Mwandishi: Florence Majani(Reuters)
Mhariri: Iddi Sessanga