1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mji wa Palmyra watekwa na magaidi

Admin.WagnerD21 Mei 2015

Wapiganaji wa dola la Kiislamu wameingia kwenye mji wa kale wa Palmyra na wameliteka jengo la makao makuu ya usalama wa nchi. Mkuu wa turathi za kale ametoa mwito wa kuunusuru mji huo..

https://p.dw.com/p/1FTUC
Mji wa kale wa Palmyra nchini Syria
Mji wa kale wa Palmyra nchini SyriaPicha: picture-alliance/dpa/Scholz

Mkurugenzi wa asasi inayofuatilia haki za binadamu nchini Syria amesema wapiganaji wa dola la Kiislamu kwa mara nyingine wameingia kaskazini mwa mji wa Tadmur . Mkurugenzi huyo Rami Abdel Rahman amesema wapiganaji wa dola la kiislamu pia wamekiteka kituo cha ukaguzi katika mji huo wa Tadmur.

Magaidi wa dola la Kiislamu wameingia katika mji wa kale wa Palmyra baada ya mapigano makali na majeshi ya serikali ya Syria, kaskazini na mashariki ya mji huo.

Jumamosi iliyopita wapiganaji wa dola la kiislamu wailiteka sehemu kubwa ya vitongoji vya kaskazini mwa mji wa Palmyra lakini walitimulia haraka na majeshi ya Syria. Mapigano yalitanda leo karibu na majengo ya usalama wa nchi kaskazini mwa mji wa Palmyra na karibu na jela ya mji.

Mwito wa kuukoa mji wa Palmyra watolewa

Mkuu wa turathi za kale katika mji wa Palmyra ametoa mwito kwa majeshi ya Syria, wapinzani na kwa jumuiya ya kimataifa wa kuulinda na kuuokoa mji huo. Mashambulio ya wapiganaji wa dola la kiislamu kwenye sehemu za turathi katika mji wa Palmyra yalianza wiki moja iliyopita, na watu zaidi ya 350 wameshauawa.

Mwanaharakati mmoja anaetokea kwenye mji wa Palmyra amesema sasa pana uhaba wa chakula katika mji huo na kwamba huduma ya nishati ya umeme inakatika katika. Amearifu kwamba idadi kubwa ya wenyeji wamegeuka wakimbizi wa ndani na wengi wanalala barabarani.

Hapo juzi wapiganaji wa linaloitwa dola la Kiislamu waliviteka visima viwili vya mafuta kaskazini mwa mji wa Palmyra. Visima hivyo vilikuwa vinatumiwa na serikali ya Syria kutoa nishati ya umeme kwa ajili ya watu walioko katika sehemu zinazodhibitwa na serikali hiyo.

Maafisa wanaohusika na turathi za kale sasa wanahofia kwamba wapiganaji wa dola la kiislamu wanakusudia kuziteketeza turathi za utamaduni ulioutangulia Uislamu .ikiwa pamoja ngome za kale kasri ,na mitaa iliyopambwa kwa safu za nguzo.

Mji wa Palmyra ,pia ni muhimu kijografia kwa sababu ya kuwa na barabara zinazoelekea katika miji ya ,Damascus na Homs , na pia barabara inayoelekea Iraq.

Wakati huo huo msemaji wa serikali ya Ufaransa amefahamisha kwamba mkutano wa kimataifa juu ya migogoro ya nchini Iraq na Syria utafanyika tarehe 2 mjini Paris.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius alitangaza kwenye mkutano wa baraza la mawaziri kwamba mkutano, utakaozijadili hali zote za nchini Syria na Iraq utafanyika mjini Paris. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry pia anatarajiwa kuhudhuria mkutano huo.

Mwandishi: Mtullya Abdu/dpa, afp,

Mhariri: Mohammed Khelef