1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafunzo ya Kijerumani yatumika kama silaha ya kisiasa Poland

9 Agosti 2023

Jamii ya wachache ya raia wa Poland wenye asili ya Ujerumani wameghadhibishwa na uamuzi wa serikali ya Poland ya kupunguza muda wa somo la lugha ya kijerumani kwenye shule za nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4Uxy7
Polen Plakat im Rahmen der Aktion der deutschen Minderheit in Polen
Bango mojawapo huko OpolePicha: VdG

Jamii hiyo inauzingatia uamuzi huo kama njama inayotumiwa na chama tawala nchini Poland katika kampeni yake ya kuchaguliwa tena katika uchaguzi wa bunge baadaye mwaka huu.

Kiasi wiki tatu zilizopita, mabango makubwa yaliyobeba ujumbe unaosomeka "Warudishieni watoto wetu lugha yao!" yalianza kuonekana pembezoni mwa barabara za jimbo la Opole la kusini magharibi mwa Poland.

Ndani ya kipindi hicho hicho, mabango yenye ujumbe sawa na huo yalionekana yametundikwa kwenye nyumba za watu binafsi kwenye jimbo hilo.

Mabango hayo yanamwonesha mvulana akiwa amefunika mdomo wake kwa mkono na ujumbe unaosomeka "Moja siyo sawa na tatu" na "Kujifunza Lugha Siyo Siasa".

Mabango na ujumbe huo ni sehemu ya ukosoaji mkali unaoiandama serikali ya Poland kutoka jamii ya raia wa taifa hilo wenye asili ya kijerumani waliokasirishwa na uamuzi wa kupunguzwa muda wa mafunzo ya lugha ya kijerumani mashuleni kutoka vipindi vitatu kwa wiki hadi kimoja pekee.

Baada ya mfululizo wa maandamano yaliyotangulia, Waziri wa Elimu wa Poland Przemyslaw Czarnek aliahidi kubadili uamuzi huo mwezi Januari mwaka huu, lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika.

Hasira na kuvunjwa moyo miongoni mwa jamii ya wenye asili ya Ujerumani

Takwimu rasmi zinaonesha, karibu raia 140,000 wa Poland wanajitambulisha kuwa na asili ya Ujerumani. Lakini kwa mujibu wa Asasi ya Jamii ya Wajerumani nchini Poland (VdG), zaidi ya raia 300,000 wa Poland wana nasaba na Ujerumani.

Wengi wao wanaishi katika jimbo la Opole, ukweli unaodhihirisha kwani hasira ni kubwa kutoka eneo hilo ambalo wakaazi wake wameumizwa na kupunguzwa kwa muda wa watoto kujifunza kijerumani.

Karte Polen Oppeln Grodisko EN

Jimbo hilo limekuwa sehemu ya Poland tangu kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia mnamo mwaka 1945.

Karibu watoto 55,000 wa jimbo hilo wameathirika na kupunguzwa huko kwa muda wa masomo ya lugha. Hayo ni kulingana na kiongozi wa asasi ya VdG, Rafal Bartek.

"Kwa maoni yangu, hili liliamuliwa chini ya mtizamo dhaifu wa kisiasa kwamba watoto wanaweza kutumika kisiasa," amesema alipozungumza na DW.

Bartek ameendelea kusema kwamba uamuzi wa serikali ulikuwa kwa jumla ni wa kisiasa na ni sehemu ya kampeni chafu ya kuipinga Ujerumani kuelekea uchaguzi wa bunge utakaofanyika msimu wa mapukutiko mwaka huu.

"Waziri Czarnek aliamini anaweza kuiadhibu serikali mjini Berlin kwa uamuzi huo kwa hoja kwamba hakuna usawa katika ufadhili unaotolewa na Poland kuendeleza lugha ya kijerumani nchini humo ikilinganishwa na Ujerumani inavyofadhili mafunzo ya utamaduni wa Kipoland".

Chama tawala nchini Poland cha (PiS) mara kadhaa kimeituhumu serikali ya Ujerumani kwa kutotoa kipaumbele na usawa kwa raia wenye asili ya Poland.

Madai hayo ya Bartek yalijibiwa na Waziri wa Elimu wa Poland kupitia mtandao wa X akisema "Iwapo kutumia Zloty (sarafu ya Poland) milioni 120 kila mwaka kufadhili ufundishaji Kijerumani kwa wakaazi wa asili ni ubaguzi, mtu atasema vipi kwa kiwango sifuri ambacho Ujerumani inatoa kuendeleza utamaduni wa Wapoland nchini Ujerumani."