Maendeleo endelevu kufadhiliwa kwa miaka 15 ijayo
17 Julai 2015Makubaliano hayo yanatoa nafasi kwa Umoja wa Mataifa kuendelea na malengo ya maendeleo endelevu yatakayoanzia mwaka wa 2015 hadi mwaka wa 2030, ambayo yataidhinishwa rasmi mwezi Septemba mjini New York Marekani.
Malengo yote yanafikia 17 kuanzia kumaliza njaa na umasikini, usawa wa kijinsia, namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kuboresha viwango vya elimu hadi kupatikana kwa nishati endelevu.
Hata hivyo katika makubaliano hayo nchi fadhili wamethibitisha kuwa wanalenga kuweka kando asilimia 0.7 ya mapato jumla ya kitaifa katika shughuli za maendeleo.
Mafanikio hayo yaliopatikana katika mkutano wa siku nne mjini Addis Ababa Ethiopia, yalifuatiwa na mikutano kadhaa ya aina hiyo mjini Monterrey, nchini Mexico mwaka wa 2002 na mjini Doha mwaka wa 2008, huku Umoja wa Mataifa ukiweka malengo ya kufadhili mipango hiyo endelevu.
Kulingana na Umoja huo pengo lililokuweko la uwekezaji katika sekta muhimu ya maendeleo endelevu kwa mataifa yanayoendelea linafikia dola trilioni 2.5 kila mwaka.
Umoja wa Mataifa wapongeza makubaliano yaliofikiwa Addis Ababa
"Nazipongeza nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kwa kupitisha ajenda ya mkutano wa Addis Ababa," alisema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon. Ameongeza kusema kile kilichoafikiwa ni hatua moja mbele ya kujenga dunia yenye mafanikio na heshima kwa wote.
Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema hatua hiyo pia itafufua ushirikiano wa maendeleo, italeta msingi imara wa utekelezwaji wa ajenda za maendeleo kuanzia mwaka huu wa 2015 na kutoa muongozo kwa wadau wote kwa uwekezaji wao kwa watu na dunia wakati wanapohitajika.
Hata hivyo baadhi ya makundi ya wafadhili yalivunjika moyo namna mkutano huo ulivyoshindwa kuunda mamlaka ya kodi ya Umoja wa Mataifa. shirika la ActionAid limesema nchi zinazoendelea zinapoteza mabilioni ya dola kila mwaka kutokana na wakwepa kodi, na hawapewi sauti sawa katika kupitisha maamuzi. Shirika hilo limesema fedha zinazopotezwa zingelitumiwa na serikali kutoa huduma nyengine muhimu.
Mashirika hayo yalitaka bodi inayosimamiwa na Umoja wa Mataifa itakayokuwa na jukumu la kuangalia kanuni mpya za kimataifa kuundwa na kuchukua nafasi ya hali ilivyo kwa sasa mbapo masuala kama hyo ya fedha yanashughulikiwa na Shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo OECD. Nchi tajiri zilizoongozwa na Uingereza na Marekani walipinga kuundwa kwa bodi hiyo ya kodi ya Umoja wa Mataifa.
Muandishi Amina AbubakarAFP/AP
Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman