Maduro ashinda uchaguzi Venezuela
21 Mei 2018Ni matokeo ambayo hayakuwashangaza watu kwa sababu chama kikuu cha upinzani kiliususia uchaguzi huo, na kisha, wapinzani wawili wakuu wakazuiwa kugombea. Na siyo hayo tu, kwa sababu hata tume ya uchaguzi inaripotiwa kuendeshwa na washirika wa karibu wa Rais Nicolas Maduro.
Tume hiyo imesema Maduro aliungwa mkono kwa kura milioni 5.8 ambazo ni sawa na asilimia 67.7, akifuatiwa kwa mbali na Henri Falcon, gavana wa zamani wa jimbo ambaye alikihama chama tawala cha kisoshalisti mwaka 2010, aliyepata kura milioni 1.8, sawa na asilimia 21.2. Katika nafasi ya tatu yuko mhubiri wa kievanjelisti Javier Bertucci, aliyeambulia asilimia 11 ya kura zilizopigwa.
Akiuhutubia umati wa wafuasi wake baada ya kutangazwa mshindi, Rais Maduro alisema wapinzani wake walijidanganya sana kuhusu uwezo wake na kuwashukuru waliomchagua.
''Asante sana kwa kushinda manyanyaso mengi na kuupuza uongo mwingi. Asante kwa kushiriki katika mapambano mengi na asante kwa kunifanya rais wa Jamhuri ya Kibolivari ya Venezuela, kwa muhula wa 2019 hadi 2025. Asante watu wapendwa wa Venezuela''. Alisema Maduro.
Uitikiaji wa chini mno
Uchaguzi huo wa jana Jumapili uliitikiwa kwa kiwango cha chini, ambacho tume ya uchaguzi imesema kilikuwa asilimia 46.1, lakini wapinzani wakiweka makadirio yao kuwa asilimia chini ya 30. Chanzo kutoka tume ya uchaguzi kimeliambia shirika la habari la Reuters kuwa asilimia 32.3 ya watu wenye sifa za kupiga kura ndio waliokuwa wamefika vituoni hadi saa kumi na mbili jioni.
Wakati Rais Maduro na kambi yake wakisherehekea, wapinzani wanalalamika. Henri Falcon aliyeshika katika nafasi ya pili amesema hakuna shaka lolote kwamba uchaguzi huo ulikosa sifa za kuwa wenye uwazi na wa kuaminika.
Alisema, ''Katika hali kama hii, ni wajibu wetu kulaani kwa sababu makubaliano yaliyosainiwa hayakuheshimiwa, na kwa hiyo, hatuutambui mchakato huu wa uchaguzi kuwa halali. Kwetu na kama hakuna uchaguzi uliofanyika. Uchaguzi mpya unahitajika kuandaliwa nchini Venezuela.''
Mkakati uliokwenda vibaya
Maduro alikuwa amemkaribisha Falcon kusimama dhidi yake, hali ambayo iliufanya uchaguzi huo uliosusia na wapinzani wengine kuwa na thamani. Hatua ya Falcon kuulani mara moja, ni pigo kwa mkakati wa serikali ya Maduro. Falcon alisema wapiga kura wengi masikini walitakiwa kuzipiga picha kadi zao za kupiga kura katika vituo mahema ya wafuasi wa Maduro waliokuwa wamepiga kambi karibu na vituo vya kupigia kura, kuthibitisha kwamba wamemchagua Maduro ili baadaye wapewe zawadi, Falcon amesema hiyo haikuwa tofauti na kuziuza kura zao.
Katika ishara kwamba muhula huu mpya wa Rais Maduro utakabiliwa na changamoto kali, utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump umesema hautautambua uchaguzi huo, na unapanga kuiwekea vikwazo sekta ya mafuta ya nchi hiyo. Kitisho hicho cha Marekani ni kama msumari mwingine kwenye jeneza la uchumi wa Venezuela ambao tayari umeporomoka.
Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, afpe
Mhariri: Grace Patricia Kabogo