1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Venezuela yadai raia wake wanataka kurudi nyumbani

Yusra Buwayhid
30 Agosti 2018

Serikali ya Venezuela ya Rais Nicolas Maduro imedai kwamba maelfu ya raia wake wanataka kurudi nyumbani katika taifa ambalo uchumi wake umeporomoka, huku mamia wakiwa wanavuka mipaka na kukimbilia nchi jirani.

https://p.dw.com/p/341ZX
Venezuela Proteste gegen Maduro
Picha: picture-alliance/ZUMAPRESS/J.-C. Hernandez

Siku moja baada ya Maduro kuwatolea wito mamia kwa maelfu ya raia wake walioikimbia nchi hiyo inayokabiliwa na mgogoro mbaya wa kiuchumi warudi nyumbani na kuachana na kazi za kuosha vyoo nchi za nje, Waziri wa Mawasiliano wa Venezuela Jorge Rodriguez amedai kwamba Wavenezuela wameitikia wito wa rais wao.

Rodriguez ameongeza kwamba balozi za Venezuela ulimwenguni kote zinapokea maombi kutoka kwa raia wao ya kutaka kurudi nyumbani.

Jumatatu iliyopita, serikali ya Venezuela imetuma ndege ya kuwarudisha raia wake 89 kutoka Peru, ambako anasema Wavenezuela wameoneshwa ubaguzi wa rangi, dharau, mateso ya kiuchumi pamoja na kugeuzwa watumwa.

Peru hivi karibuni imeongeza udhibiti wa mpaka, na kuwataka Wavenezuela wanaokimbia umasikini nchini mwao, waonyeshe hati ya kusafiria ili waruhusiwe kuingia nchini humo, wakisema kwamba zaidi ya raia wa Venezuela 400,000 tayari wanaishi nchini Peru.

Rodriguez amezitaja nchi za Peru, Ecuador na Colombia kuwa ndiyo nchi ambako Wavenezuela wanakabiliwa na ubaguzi wa rangi pamoja na uhalifu unaotokana na ubaguzi huo.

Ameongeza kwamba serikali yake itawasilisha malalamiko rasmi katika Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wakimbizi, na kudai jawabu kutoka nchi hizo zinazowatesa raia wake.

Wanawake na watoto wako hatarini kutumbukizwa katika biashara ya ngono

Flüchtlinge aus Venezuela in Brasilien
Wahamiaji wa Venezuela wakiwa nchini BrazilPicha: DW/Y. Boechat

Wakimbizi kutoka Venezuela wakiwa wanamiminika nchi jirani, Brazil imetuma wanajaeshi zaidi katika mpaka wake, kufuatia shambulio la vurugu la mapema mwezi huu lilofanywa na raia wa Brazil na kusababisha wahamiaji 1,200 kurudi nyumbani Venezuela.

Rais wa Brazil Michel Temer amesema wanajeshi hao wametumwa mpakani kuwalinda raia wa Brazil, lakini pia raia wa Venezuela wanaoikimbia nchi yao.

Amekiambia kituo cha Redio Jornal kwamba mfumo wa kutoa tiketi utatumika kupokea wahamiaji hao wanaotoka Venezuela katika mpaka wa Brazil, ili waweze kupokea wahamiaji 100 hadi 200 kwa siku na sio idadi wanayoipokea sasa ya wahamiaji 700 hadi 800 kwa siku.

Serikali ya Brazil imesema mfumo huo utasaidia kuwapa kipaumbelea wale ambao wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu. Na isitafsiriwe kama vile Brazil inaufunga mpaka wake kwa raia wa Venezuela.

"Tutatumia juhudi zote katika vikao vyote vya kimataifa ili kuibadilisha hali hii. Tutaomba msaada katika jumuiya ya kimataifa kupitishwe hatua za kidiplomasia imara za kutatua tatizo hili ambalo chanzo chake ni siasa za ndani ya taifa moja  lakini limeenea katika mipaka ya nchi kadhaa na kutishia maelewano ya bara zima," amesema Michel Temer.

Wakati huo huo, mashirika ya misaada ya kibinadamu yamesema hapo jana kwamba wanawake na watoto wanaoihama Venezuela kutokana na kuporomoka kwa uchumi wake, wako katika hatari kubwa ya kunyanyaswa kijinsia na kutumbukizwa katika biashara haramu ya kusafirisha binadamu, wakiwa safarini wanatafuta hifadhi katika mataifa tofauti ya Amerika Kusini.

Tokea mwaka 2015, zaidi ya raia milioni 1.6 wa Venezuela wamekuwa wakilihama taifa hilo lenye utajiri wa mafuta, wengi wao wakitafuta maisha bora nchini Colombia na mataifa mengine jirani.

Umoja wa Mataifa umesema ni miongoni mwa uhamiaji mkubwa wa watu katika historia ya eneo la Amerika Kusini.

Ripoti ya utafiti iliyotolea na taasisi ya Colombia ya Ideas For Peace, FIP, inaeleza kwamba usafirishaji wa wahamiaji wa Venezuela kwa ajili ya biashara ya ngono umestawi zaidi katika mipaka wa kaskazini mwa Colombia ambako kunapatikana makundi mengi ya uhalifu pamoja na makundi ya wanamgambo.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/dpa/afp/rtre

Mhariri: Grace Patricia Kabogo