1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madaktari Sudan waandamana kupinga mashambulizi dhidi yao

17 Januari 2022

Madaktari nchini Sudan wameandamana kupinga mashambulizi wanayodai yanafanywa na maafisa wa usalama dhidi ya maafisa wa afya, wakati wa maandamano ya kudai demokrasia kufuatia mapinduzi yaliofanyika mwaka uliopita.

https://p.dw.com/p/45d3I
Sudan | Proteste in Khartoum
Picha: AFP/Getty Images

Maandamano hayo yaliofanyika jana Jumapili ndio yaliokuwa maandamano ya hivi karibuni kutokea katika taifa hilo la Kaskazini Mashariki mwa Afrika, lililokumbwa na mgogoro. Houda Ahmad  aliyeshiriki maandamano hayo mjini Khartoum amesema maafisa wa usalama wanawalenga kwa kuwarushia mabomu ya kutoa mchozi ndani ya hospitali anakofanya kazi.

Houda na wenzake waliokuwa wamebeba mabango yaliokuwa na picha za wenzao waliouwawa katika mashambulizi hayo, amedai maafisa wa usalama wamekuwa wakiwashambulia hadi katika vyumba vya wagonjwa mahututi.

soma zaidi: Marekani, Ulaya waionya Sudan kuhusu uteuzi mpya

Shirika la afya ulimwenguni WHO wiki iliyopita lilithibitisha kuwepo mashambulizi 11 nchini Sudan dhidi ya taasisi za afya tangu mwezi Novemba mwaka jana. WHO imetoa wito wa mashambulio  hayo kukomeshwa mara moja ikisema inatishia utoaji bora wa huduma ya afya inayohitajika hasa katika kipindi hiki cha janga la corona.

Shirika hilo la Afya duniani limesema virusi vya corona ni tishio kubwa kwa Sudan ambako asilimia 94 ya idadi ya watu haijachomwa chanjo dhidi ya virusi hivyo. Tayari watu 93,973 wanaugua virusi hivyo huku vifo 4000 vikiripotiwa.

Umoja wa Mataifa unaendelea kutafuta suluhu ya kudumu Sudan

USA New York | UN Hauptquartier - Voler Perthes zu Sudan
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwaajili ya Sudan Volker PerthesPicha: Loey Felipe/Xinhua/picture alliance

Wakati huo huo Sudan iliyo na idadi ya watu milioni 45 inapitia mgogoro wa kiuchumi huku hali ya maisha ikipanda maradufu. Waandamanaji walioandamana hapo jana walifunga barabara muhimu mjini Khartoum kuelezea hasira zao pia juu ya kupanda kwa bei ya umeme iliyotangazwa wiki iliyopita ambayo baadae ilisimamishwa kwa muda lakini bado haijafutiliwa mbali.

Hassan Idriss mmoja ya waandamanaji aliliambia shirika la habari la AFP kwamba waataendelea kuzuwiya magari kutumia barabara hiyo muhimu hadi pale serikali itakapofuta kabisa ongezeko hilo.

Kujiuzulu kwa Hamdok huenda kukarejesha staili ya uongozi wa Bashir

Maandamano yaliyosababishwa na mapinduzi ya kijeshi yalioongozwa na jenerali Abdel Fattah al-Burhan tarehe 25 Oktoba mwaja jana yalichelewesha hatua muhimu ya kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia iliyoanza mwaka 2019 baada ya kiongozi wa muda mrefu nchini humo Omar al Bashir kuondolewa madarakani kufuatia maandamano makubwa dhidi yake.

Kwa sasa Umoja wa Mataifa unaendelea na juhudi ya kuandaa mazungumzo kati ya jeshi na viongozi wa kiraia na makundi yanayodai demokrasia ili kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro wa Sudan.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwaajili ya Sudan Volker Perthes alitangaza hilo wiki iliyopita akisema muda umefika wa kumaliza vurugu na kuingia katika njia ya maridhiano.

Chanzo: ap/afp