1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madagascar wapiga kura duru ya pili ya uchaguzi

Yusra Buwayhid
19 Desemba 2018

Raia wa Madagascar Jumatano wameanza kupiga kura kote katika kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi, ili kumchagua rais mpya katika duru ya pili ya uchaguzi unaowakutanisha viongozi wawili wa zamani wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/3AMLW
Madagaskar, Antananarivo: Wahlen des Präsidenten
Picha: picture-alliance/AP/K. Dhanji

Andry Rajoelina mwenye umri wa miaka 44 na ambaye aliwahi kuwa rais kati ya mwaka 2009 hadi 2014, alipata asilimia 39 ya kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi mwezi Novemba, huku Marc Ravalomanana mwenye umri wa miaka 69, na aliyekuwa rais wa kisiwa hicho kutoka mwaka 2002 hadi 2009 alipata asilimia 35 ya kura zote zilizopigwa wakati huo.

Wanakutana tena kwa mara ya kwanza tokea mgogoro wa kisiasa wa mwaka 2009 ulipomlazimisha Ravalomanana kuondoka madarakani na kupokewa wadhifa huo na Rajoelina. Wanasiasa wote wawili wamesema watakubali matokeo ya duru hiyo ya pili ya uchaguzi.

Madagaskar, Antananarivo: Wahlen des Präsidenten
Andry Rajoelina akipig kura mjini AntananarivoPicha: picture-alliance/AP/K. Dhanji

Rajoelina ajiamini

Baada ya kupiga kura yake katika mji mkuu wa Antananarivo, Rajoelina amesema anajiamini kushinda katika uchaguzi huo.

"Binafsi, ninajiamini. Na nina imani wananchi wa Madagascar wataamua hatimaye nani wanamtaka kuiongoza nchi. Nawaomba kwa mara nyingine tena wananchi wa Madagascar kujitokeza kwa idadi kubwa kupiga kura, sasa hivi, hamna sababu ya kungoja hadi dakika ya mwisho kupiga kura," amesema Andry Rajoelina, mgombea urais katika uchaguzi wa Madagascar.

Watu milioni kumi wamejiandikisha kupiga kura katika nchi hiyo ambayo zamani ilikuwa koloni la Ufaransa, na inatajwa na Benki ya Dunia kuwa miongoni mwa mataifa masikini duniani, ingawa ina utajiri wa viumbe hai pamoja na aina mbalimbali za miti. Ni taifa lenye mazingira  ya kiikolojia yanayovutia.

Madagaskar Landschaft - Namorona Fluss im Ranomafana Nationalpark
Mandhari ya kuvutia ya MadagascarPicha: Imago/robertharding

Zaidi ya thuluthi mbili ya idadi nzima ya watu milioni 25 nchini humo wanaishi katika umasikini wa kiwango cha juu, huku rushwa ikitajwa kuwa imetawala katika kisiwa hicho. Kipindi cha kampeni kilimalizika kwa amani. Mji wa Antananarivo ulichangamka katika siku za mwisho za kampeni. T-shati za rangi ya machungwa za wafuasi wa Rajoelina na nyeupe kwa kijani za wafuasi wa Ravalomanana zilikuwa zikioneka kila kona ya mji huo. Matokeo ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutolewa ndani ya wiki hii.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/ap

Mhariri: Daniel Gakuba