Macron aangazia kurekebisha uhusiano na Algeria
26 Agosti 2022Ziara hiyo ya siku tatu inafuatia miezi kadhaa ya mvutano kati ya Ufaransa na Algeria, ambayo mapema mwaka huu iliadhimisha miongo sita ya uhuru kufuatia miaka 132 ya utawala wa Ufaransa. Ziara hiyo pia inakuja wakati mataifa ya Ulaya yakipambana kubadilisha uagizaji wa nishati kutoka Urusi ikiwa ni pamoja na bidhaa kutoka Algeria, ambayo ni muuzaji mkuu wa gesi barani Afrika, ambayo kwa upande wake inatafuta jukumu kubwa zaidi la kikanda.
Siku ya Alhamisi, Macron alikuwa ametangaza ukurusa mpya wa uhusiano kati ya nchi hiyo mbili baada ya kukutana na rais Abdelmadjid Tebboune na kutangaza kuundwa kwa tume ya pamoja ya wanahistoria kuchunguza kipindi cha ukoloni na vita vikali vya miaka minane vilivyomaliza kipindi hicho kilichosababisha vifo vya maelfu ya watu.
Siku ya Ijumaa, rais huyo amesema kuwa Algeria ilikuwa imelisaidia bara Ulaya kupanua usambazaji wake wa nishati kwa kusukuma gesi zaidi nchini Italia, ambayo mwezi uliopita ilitia saini makubaliano ya kuagiza nishati zaidi kupitia bomba la chini ya bahari kutoka pwani ya Afrika Kaskazini.
Macron apuuza madai kwamba Ufaransa na Italia ziko katika ushindani
Akipuuzilia mbali madai kwamba Italia na Ufaransa zilikuwa katika ushindani wa gesi ya Algeria, Macron alipongeza makubaliano hayo. Pia alipuuzilia mbali madai kwamba Italia na Ufaransa ziko katika ushindani, akibainisha kuwa Ufaransa inategemea tu gesi asilia kwa sehemu ndogo ya mchanganyiko wake wa nishati. Macron pia amesema walijadili kwa uhuru hali ya haki za binadamu nchini Algeria na rais Tebboune, ambaye alisema anachukulia kwa makini masuala hayo. Macron ameongeza kuwa masuala hayo yatatatuliwa kwa heshima kamili ya uhuru wa Algeria. Pia aliwahimiza vijana nchini Algeria kutotekwa na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na mataifa ya kigeni ikiwemo Urusi na China.
Kulingana na Tebboune, Viongozi hao wawili pia walizungumzia kuhusu jinsi ya kuleta uthabiti nchini Libya, katika eneo la Sahel na eneo linalozozaniwa la Sahara Magharibi. Macron pia alitarajiwa kuzuru msikiti mkuu wa Algiers Ijumaa kabla ya kuelekea mji wa pili wa Oran kwaajili ya masuala ya sanaa.