1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron akabiliwa na vita vikali vya udhibiti wa bunge

19 Juni 2022

Raia wa Ufaransa wanateremka vituoni leo kushiriki duru ya pili ya uchaguzi wa bunge ambao utatoa mwelekeo wa utawala wa rais Emmanuel Macron aliyechaguliwa kuiongoza nchi hiyo kwa muhula wa pili mnamo mwezi Aprili

https://p.dw.com/p/4Cu3c
Frankreich | Wahlen 2022 | Parlament
Picha: Jean-Francois Badias/AP Photo/picture alliance

Wapiga kura nchini Ufaransa wanamiminika vituoni katika duru ya mwisho ya uchaguzi wa bunge, huku muungano wa siasa za wastani wa rais wa Emmanuel Macron ukilenga kuzuia upinzani wa muungano wa siasa za mrengo wa kushoto ulioundwa hivi karibuni.

Soma zaidi: Kambi ya rais Macron yatwaa ushindi uchaguzi wa bunge

Uchaguzi huo utakuwa muhimu kwa ajenda ya muhula wa pili wa Macron kufuatia ushindi wake wa Aprili, huku rais huyo mwenye umri wa miaka 44 akihitaji wingi wa kura ili kufanikisha mageuzi yake aliyoahidi ya kupunguza kodi, ustawi wa jamii na kuongeza umri wa kustaafu.

Matokeo ya uchunguzi wa maoni yanaashiria kuwa muungano wake wa "Ensemble" au "Pamoja" unaelekea kuwa chama kikubwa katika Bunge lijalo la Kitaifa, lakini hautapata viti 289 vinavyohitajika ili kuwa na wingi wa viti.

Frankreich Parlamentswahl | Emmauel Macron
Macron anatafuta wingi wa viti bungeniPicha: Johan Ben Azzouz/MAXPPP/dpa/picture alliance

Muungano mpya wa mrengo wa kushoto NUPES umataraji kusababisha mshangao, huku chama hicho chana nyekundu na kijani kikiahidi kuipinga ajenda ya Macron baada ya kuungana nyuma ya mwanasiasa mkongwe mwenye umri wa miaka 70 Jean-Luc Melenchon.

Kiongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia Marine Le Pen pia anawinda viti kadhaa kwa ajili ya chama chake cha National Rally, ambacho kilikuwa tu na viti vinane katika bunge linalomaliza muhula wake.

Soma pia: Maoni: Ushindi wa Macron fursa kwa Ulaya

Macron alikatishwa tamaa na matokeo ya mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya duru ya kwanza ya upigaji kura kuonyesha Ensemble na NUPES wakitoshana kwa asilimia 26 ya kura.

Kuongezeka kwa mfumuko wa bei, kampeni zisizo na mvuto kutoka kwa Waziri Mkuu mpya Elisabeth Borne, na tabia ya ukali ya Macron vyote vimeonekana kama sababu za kutofanya vizuri. Duru ya kwanza ya iliwachuja wagombea- katika mengi ya majimbo 577 ya ubunge nchini humo na kubaki na wawili ambao watapambana ana kwa ana leo.

Tafiti za maoni Ijumaa ziliashiria kuwa washirika wa chama cha Ensemble cha Macron watapata viti kati ya 255 – 305 katika uchaguzi wa leo.

Jean-Luc Melenchon
Jean-Luc Melenchon anatumai kuwa waziri mkuuPicha: Sarah Meyssonnier/REUTERS

NUPES watapata karibu 140-200, na kuwafanya kuwa kundi kubwa kabisa la upinzani, wakati chama cha National Rally cha Le Pen kikionekana kupata karibu viti 20 - 45. Kama watapata Zaidi ya viti 15, wabunge wa Le Pen wataweza kuunda kundi rasmi bungeni, hali itakayowapa muonekano Zaidi na raslimali.

Macron alielekea Ukraine mapema wiki hii, akitumai kuwakumbusha wapiga kura kuhusu sifa zake za sera yake ya kigeni na mojawapo ya udhaifu unaoonekana wa Melenchon – maoni yake ya kuipinga Jumuiya ya Kujihami ya NATO na kuupinga Umoja wa Ulaya katika wakati wa vita barani Ulaya.

Soma pia: Macron ampiku Le Pen na kupata muhula wa pili

Imekuwa miaka 20 tangu Ufaransa mara ya mwisho ilikuwa na rais na Waziri mkuu kutoka vyama tofauti, wakati kiongozi wa siasa za mrengo wa kulia Jacques Chirac alilazimika kufanya kazi na bunge lililotawaliwa na Wasoshalisti chini ya Waziri mkuu Lionel Jospin.

afp/reuters