1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machafuko kisiwani Madagascar

Oumilkher Hamidou26 Januari 2009

Upande wea upinzani kisiwani Madagascar walalamika dhidi ya serikali

https://p.dw.com/p/GgWa
Rais wa Madagascar Marc RavalomananaPicha: picture-alliance/ dpa




Meya wa mji mkuu wa Madagascar,Antananarivo,Andry RAJOELINA,mpinzani mkubwa wa rais RAVALOMANANA amezidisha makali ya mvutano dhidi ya serikali kwa kuwakusanya maelfu ya wafuasi wake hii leo katika maandamano yaliyogeuka kua matumizi ya nguvu.


Jengo la Radio ya taifa Radio National Malgache-RNM iliyoko katika eneo la kati la mji mkuu Antananarivo limevamia,na baadae kutiwa moto.


Wafanyafujo hao ni sehemu ya maelfu ya wafuasi wa upande wa upinzani waliokusanyika leo asubuhi katika uwanja wa May 13-kitovu cha malalamiko ya wabuki,wakijibu mwito wa mgomo jumla uliotolewa ijumaa iliyopita na Meya Andry Rajoelina anaekosoa kile anachokiita "uimla unaoendelea Madagascar."


Usafiri katika mji mkuu wa Madagascar umeparaganyika kutokana na izuwizi vilivyowekwa majiani.


Licha ya onyo la serikali,meya wa Antananarivo Andry Rajoelina amemlaumu rais Marc Ravalomanana na serikali yake anayoitaka kua ni ya kimabavu na kusema tunanukuu:"Madaraka yanamilikiwa na umma.Unaweza kunyakua madaraka hayo.Kila saa inapopita,serikali inadhihirisha uimla" mwisho wa kumnukuu  meya huyo kijana wa miaka 34 aliyewataka wafuasi wa upande wa upinzani wateremke tena majiani kesho.


Andry Rajoelina,ambae pia ni mfanyabiashara amekua akizozana na utawala wa rais Ravalomanana tangu alipochaguliwa kua meya wa Antananarivo December mwaka 2007.


Mzozano wao umezidi makali baada ya serikali kuamua kukifunga kituo cha televisheni cha kibinafsi  Viva,december 13 mwaka jana-baada ya kituo hicho kufanya mahojiano pamoja na rais wa zamani Didier Ratsiraka anaeishi uhamishoni nchini Ufaransa tangu mwaka 2002.


Rais Marc Ravalomanana amefupisha ziara yake nchi za nje na kurejea nyumbani jana,akisema "anataka kurejesha nidhamu na kuihami Jamhuri".


"Mwito wa kutoheshimu amri ya serikali uliotolewa na meya wa Antananarivo ni sawa na njama ya mapinduzi na unavuruga maadili ya kikatiba."Amesema hayo rais Marc Ravalomanana katika taarifa yake .


Ikiwa chanzo cha mtafaruku ni kufungwa kituo cha televisheni ya kibinafsi ya Viva,meya Rajoelina anakosoa pia ukosefu wa haki ya mtu kutoa maoni yake na ukosefu wa demokrasia katika kisiwa hicho kikuu pamoja na kunyakuliwa ardhi za wabuki kwa masilahi ya mradi mkubwa wa kilimo unaosimamiwa na shirika la Korea ya kusini-Daewoo.


Upande wa upinzani kisiwani Madagascar unakosowa pia makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya serikali  na mashirika ya kigeni ,ikihusika pia sekta ya maadini katika wakati ambapo nchi hiyo inazidi kudidimia katika bahari ya umaskini.