1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tabianchi na migogoro ni kitisho kwa vita dhidi ya Ukimwi

19 Septemba 2024

Shirika la kimataifa la The Global Fund limetahadharisha kuwa mabadiliko ya tabianchi na migogoro inatishia kurudisha nyuma vita dhidi ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria.

https://p.dw.com/p/4kpBV
Ujerumani Munich 2024 | Mlango wa Mkutano wa Kimataifa wa UKIMWI kabla ya kufunguliwa na Kansela Scholz
Ujerumani Munich 2024, Mlango wa Mkutano wa Kimataifa wa UKIMWI ikiwa kabla ya ufunguzi wa mkutano huo.Picha: Sabine Dobel/dpa/picture alliance

Shirika hilo lenye makao makuu yake mjini Geneva limesema dunia imefanikiwa kujinasua kwa kiasi kikubwa kutoka kwenye janga la ugonjwa wa Covid-19. Hata hivyo kwa wakati huu dunia inakabiliwa na migogoro ya kisiasa, kuporomoka kwa demokrasia na haki za binadamu, kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia, mabadiliko ya tabia nchi, ongezeko la madeni na matatizo ya kiuchumi. The Global Fund imesema katika ripoti yake ya kila mwaka kwamba changamoto hizo zinawaweka watu maskini na jamii zilizotengwa katika hatari kubwa ya kupata magonjwa ya kuambukiza. Shirika hilo la kimataifa limewekeza zaidi ya dola bilioni tano mnamo mwaka 2023 katika vita dhidi ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria, magonjwa ambayo huua mamia kwa maelfu ya watu kila mwaka na kuathiri mamilioni ya wengine.