1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafuriko yasababisha watu 100,000 kutokuwa na makazi Burundi

20 Septemba 2021

Ripoti ya shirika Save the Children imesema majanga ya asili ambayo yamesababishwa na mabadiliko ya tabia nchi ya miaka ya hivi karibuni yamewalazimisha watu zaidi ya 100,000 nchini Burundi kuachwa bila ya makazi.

https://p.dw.com/p/40XkI
Tansania Burundis Flüchtlinge
Picha: Tchandrou Nitaga/AFP/Getty Images

 

Ripoti hiyo inasema mabadiliko ya tabia nchi ni jambo la kushtusha na sio migogoro ambayo imekuwa chanzo kikubwa katika kuwafanya wengi wayakimbie makazi yao kwa taifa hilo, lisilo na bandari na lililo katika Afrika Mashariki, ambalo pia wakazi wake wengi wapo katika maeneo ya vijijini.

Save the Children imesema zaidi ya asilimia 84 ya watu ambao wameachwa bila ya makazi ndani ya Burundi, imetokana na majanga asilia kuliko migogoro, na mengi  yametokana na kufurika kwa Ziwa Tanganyika, ambalo ni la pili kwa ukubwa barani Afrika.

Save the Children: Watoto wameathirika zaidi

TABLEAU | Weltflüchtlingstag 20.6.2021 Bildergalerie
Watu wasio na makazi kutoka BurundiPicha: Khalil Senosi/picture alliance/AP Photo

Kadhia hiyo inatajwa kuwaathiri zaidi watoto ambapo Save the Children linakadiria 7,200 miongoni mwa waathirika au asilimia 7 ikiwa ni watoto wa chini ya umri wa mwaka mmoja. Watoto wa wakubwa wanashindwa kuhudhuria masomo, huku wakiishi katika mazingira magumu ya kupata mlo mmoja kwa siku. Mtoto Arielle, wa umri wa miaka 17, ambae nyumba yao ilisombwa na mafuriko usiku wa manene baada ya kuongeza kwa maji, aliliambia shirika Save the Chidren, anahangaika kupata fedha ya kujikimu ya kiasdi cha japo euro moja kwa siku  kwa kufanya kazi ya kurundika matofali.

Anasema anakula kila siku, ingawa kuna baadhi ya siku anakosa hata kupata mlo mmoja. Wakulima ambao kwa sasa hawana makazi waliliambia shirika hilo kwamba majanga ya mafuriko yameongezeka zaidi katika siku za hivi karibuni. Marie, ni mama wa watoto watatu na amenukuliwa na Save the Chidren akisema "Hali ya mafuriko imekuwa mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Kipindi hiki mafuriko yanaongezeka na hayapungui. Nahofia wanangu kupoteza maisha kwa njaa."

Jumuiya ya kimataifa imeonekana kama imeisahahu Burundi

Maggie Korde, ambae ni mwakilishi mkazi wa Save the Chidren katika mataifa ya Burundi la Rwanda ameonya kwamba dunia inaonekana kama imeisahau Burundi, na kwamba hivi sasa inabeba mzigo mkubwa wa matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi, ambapo watoto wamekuwa waathirika wakubwa.

Amesema wanashuhuhudia familia ambazo awali zilikuwa zenye makazi madhubuti, watoto wote wanakwenda shule na wazazi wawili wanaofanya kazi kwa sasa wanaishi katika mahema, hawana ajira, hakuna chakula na watatoto wanapaswa kufanya kazi kwa dola moja kwa siku ili waweze kufanikisha mlo kwa familia zao.

Ripoti hii mpya imetolewa katika kipindi cha takribani miaka miwili baada ya mvua kumbwa kunyesha katika eneo la Afrika Mashariki, ambayo imeathiri karibu watu milioni mbili na wemngine 265 kupoteza maisha. Ripoti nyingine ya kisayansi ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa Juni inatabiri mafuriko yatasababisha watu milioni 2.7 kutokuwa na makazi kwa mwaka barani Afrika na milioni 85 kutokuwa na makazi ifikapo 2050.

Chanzo:AFP