Maaskofu wa Katoliki Afrika wapinga kubariki ndoa za mashoga
12 Januari 2024Maaskofu wa Kikatoliki wa Afrika wamesema kuwa idhini iliyotolewa hivi karibuni na Vatican ya kubariki wapenzi wa jinsia moja haikuwa sahihi kwa bara hilo kwani inakinzana na maadili na utamaduni wa mwafrika.
Kongamano la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagascar SECAM, limesema katika taarifa yake kuwa mafundisho ya kanisa kuhusu ndoa na kujamiiana bado hayajabadilika.
Maaskofu hao wamesisitiza kwamba hawatobariki ndoa za mashoga kwani kwa kufanya hivyo watazusha taharuki miongoni mwa waumini. Mwezi uliopita kanisa katoliki lilisema kuwa mapadri wanaweza kubariki wapenzi wa jinsia moja chini ya mazingira fulani.
Uamuzi huo wa Vatican umepingwa vikali na nchi za Malawi, Nigeria, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ushoga bado ni kinyume cha sheria katika nchi nyingi za Kiafrika.