Maandamano ya upinzani yavurugwa Zimbabwe
16 Agosti 2019Licha ya amri ya kutofanyika maandamano ya leo iliyotolewa na mahakama kuu nchini Zimbabwe, mamia ya watu bado walijitokeza barabarani kuandamana kupinga hali ya uchumi na serikali ya rais Mnangagwa.
Kiongozi wa chama cha upinzani MDC Nelson Chamisa kilichoandaa maandamano hayo, amesema watu takriban saba wamejeruhiwa, mmoja akiwa hali mahututi na wengine takriban 80 wamekamatwa.
Licha ya hayo Chamisa amesema hawatopumzika hadi watakapofanikiwa kuwa na serikali ya watu wa zimbabwe. Polisi waliwarushia vitoa machozi waandamanaji waliyokuwa wamekusanyika katika eneo moja mjini Harare.
Polisi hao walitumia marungu kuwapiga watu na mwanamke mmoja alizirai barabarani baada ya kipigo kutoka kwa polisi.
Mwanamke huyo pamoja na wengine walipata matibabu ya dharura kabla ya kuchukuliwa na magari ya kubebea wagonjwa na kukimbizwa hospitalini.
Makundi ya vijana wadogo walikusanyika mjini humo wakiimba kwa sauti nyimbo za kuipinga serikali. "Usinililie nitakapokufa, nimechagua kufa kwaajili za Zimbabwe" waliimba baadhi ya waandamanaji kwa lugha ya kishona kabla ya kukimbia madhila ya polisi.
Baadhi ya waandamanaji wamtaka rais Munangagwa ajiuzulu
"Tunapoteza saa nyingi kwenye milolongo ya mafuta ya petroli, hakuna pesa benki, kila kitu kimekauka, naandamana ili kuonesha kutoridhishwa na serikali hii," alisema Gideon Homwe Mmoja ya waandamanaji.
Nae Melody Gwera aliye na miaka 64 anasema yeye anaandamana dhidi ya utawala wa rais Emmerson Mnangagwa amesema ameshindwa na anapaswa kujiuzulu akisema kuwa kwa sasa hawezi kununua bidhaa muhimu kwa familia yake.
Hapo jana Kiongozi wa masuala ya vijana kutoka chama tawala cha ZANU PF Pupurai Togarepi walikionya chama cha upinzani cha MDC dhidi ya kujaribu kumuondoa madarakani rais Mnangagwa.
Raia wengi wa Zimbabwe wamechoshwa na serikali hii ya Zimbabwe iliyoahidi kuurekebisha uchumi wa nchi hiyo wakati nafasi ya rais wa muda mrefu Robert Mugabe ilipochukuliwa na rais Mnangagwa mwishoni mwa mwaka 2017.
Zimbabwe ilipitia maandamani makubwa yaliyokuwa na vutugu mapema mwaka huu baada ya serikali kupandisha zaidi ya mara mbili bei ya mafuta.
Vyanzo: afp/dpa