Maandamano ya kuipinga Rwanda yaenea mashariki mwa DRC
16 Februari 2024Maandamano ya kuipinga Rwanda na mataifa ya Magharibi yalienea jana katika mikoa ya Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Soma pia: Askari wawili wa Afrika Kusini wauawa katika mlipuko Kongo
Waandamanaji wanazishutumu nchi hizo kwa kushirikiana na kundi la waasi wa M23 ambalo limesababisha maafa katika eneo hilo. Mamia ya watu waliandamana mjini Bukavu huko Kivu Kusini, wakishinikiza kukombolewa kwa baadhi ya maeneo ya jimbo jirani la Kivu Kaskazini yanayodhibitiwa na M23.
Waandamanaji wanataka kufungwa kwa mipaka ya Rwanda na Uganda, ambayo pia inashutumiwa kwa kuwanunga mkono waasi. Pia wamehimiza juu ya kuvunjwa uhusiano wa kidiplomasia na mataifa ya Marekani, Ufaransa na Uingereza.
Maandamano mengine yalifanyika Kisangani katika jimbo la Tshopo, yakitaka kutangazwa kwa vita dhidi ya Rwanda na kuvunja uhusiano na nchi za Magharibi. Mamia ya wanawake waliandamanasiku moja kabla mjini Kinshasa wakiwa na madai sawa.