Maandamano kupinga unazi mambo leo yafanyika Marekani
13 Agosti 2018Maandamano hayo yaliyofanyika katika miji ya Charlotteville na Washington yalikuwa ya amani licha ya mtu mmoja kukamatwa mjini Washington na wengine wanne walikamatwa mjini Charlottesville.
Mjini Charlottesville mama wa mtoto aliyeuawa wakati wa maandamano yaliyofanyika katika msimu wa majira ya kiangazi mwaka jana alizuru eneo la shambulizi akisema majeraha yaliyotokana na matukio ya ubaguzi wa rangi bado hayajapona
Mjini Washington katika maeneo ya ikulu ya Marekani White House polisi kadhaa waliwadhibiti waandandamanaji wanaounga mkono siasa kali za mrengo wa kulia ili wasiwazomee waandamanaji wanaopinga uzalendo mambo leo.
Jasson Kessler, muandaaji wa maandamano ya mwaka jana ya watu wanaotetea uzalendo mambo leo aliongoza maandamano ya hapo jana aliyoyaita haki ya mtu mweupe . Kessler katika barua yake ya kuomba kibali cha maandamano alisema alitarajia watu 100 hadi 400 wajitokeze kushiriki lakini hata hivyo ni watu waliojitokeza walikuwa wachache sana wakikadiriwa kufikia 20.
Hata hivyo maandamano hayo yaliingiliwa na maelfu ya waandamanaji waliokuwa wakipinga uzalendo mambo leo waliokuwa wamekusanyika hapo kabla katika viwanja vya Lafayette . Makia Green anayewakilisha kundi la watu weusi mjini Washington chini ya kauli mbiu " Maisha ya Mtu Mweusi ni MuhImu" alisikika akisema licha ya yote bado wanatambua kutokana na uzoefu wao kuwa kupinga uzalendo mambo leo ni suala lisilo itikiwa vizuri nchini humo.
Rais Donald Trump hakuwepo ikulu
Rais Donald Trump ambaye alichochea mivutano zaidi kutokana na kauli yake wakati akizungumzia vurugu za mwaka jana za Chalottesville alipozilaumu pande zote mbili safari hii hakuwa katika makazi yake ya Ikulu kwani alikuwa katika mapumziko ya kikazi mjini New Jersey katika kipindi cha zaidi ya wiki moja sasa.
Mkuu wa polisi mjini Washington Peter Newsham aliwapongeza maafisa wake kwa kufanikiwa kuzuia vurugu ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kuyatenganisha makundi hayo mawili yenye itikadi tofauti yaliyokuwa yakiandamana. Alisikika akisema wametumia utaratibu mzuri katika kulinda usalama wa watu na mali zao ikiwa ni pamoja na kuruhusu raia kutumia haki yao ya kuandamana na kujieleza.
Mapema mjini Charlottesville mama wa binti Heather Heyer aliyeuawa wakati wa maandamano ya mwaka jana alisema bado kuna mengi ya kufanya katika kuponya majeraha yaliyosababishwa na vurugu za mwaka jana. Mama huyo Suzan Bro aliweka shada la maua katika eneo ambalo vurugu zilifanyika mjini Charlottesville na kuwashukuru watu walioungana naye kumkumbuka binti yake wakati wa tukio hilo.
Alisikika akisema kuna kazi kubwa ya kufanya katika kutibu majeraha ya vurugu zinazotokana na matukio ya ubaguzi na kusema kuna haja ya kulitafutia ufumbuzia haraka tatizo hilo vinginevyo tutarejea kulekule.
Mamia ya Wanazi mamboleo, na wanachama wa kundi linaloangalia jamii ya wazungu kuwa bora zaidi la Ku Klux Klan na wengine wafuasi wa siasa za kizalendo walikusanyika katika mji wa Charlottesville Agosti 12 , 2017, kwa sehemu fulani kupinga uamuzi wa mji huo kuliondoa sanamu la kumbukumbu ya jenerali Robert E. Lee kutoka katika uwanja wa mji huo.
Makabiliano makali yalizuka baina ya waliohudhuria dhidi ya maandamano ya kupinga. Maafisa hatimaye walifanikiwa kulilazimisha kundi hilo kutawanyika, lakini ghasia zilizuka tena wakati gari ilipogonga kundi la waandamanaji.
Mwandishi: Isaac Gamba /APE
Mhariri: Josephat Charo