Maandamano duniani ukatili wa polisi; kifo cha Floyd
3 Juni 2020George Floyd mtu mweusi alifariki baada ya afisa wa kizungu kuibana shingo yake kwa goti kwa dakika kadhaa, hata baada ya kushindwa kupumua. Wakati huo huo maandamano kadhaa yamefanyika katika miji mbali mbali duniani , ikiwa ni pamoja na miji ya Ufaransa , Uholanzi, na Angentina kupinga ukatili wa polisi.
Gavana wa Minnesota Tim Walz na idara ya haki za binadamu ya Minnesota wametangaza kufungua malalamiko rasmi katika mkutano na waandishi habari jana jioni. Gavana na kamishna wa haki za binadamu Rebecca Lucero wamesema wana matumaini kufikia makubaliano na mji huo kubaini njia za muda mfupi kuangalia historia ya idara ya polisi ya ubaguzi wa rangi, na kutumia uchunguzi huo kupata suluhisho la muda mrefu kwa ajili ya mabadiliko ya mfumo.
wakati huo huo mamia kwa maelfu ya waandamanaji wanaopinga kifo cha George Floyd waliendelea kubaki katika mitaa ya mjini New York jana baada ya muda wa kuanza kwa amri ya kutotembea usiku kuanzia saa mbili usiku saa za Marekani, amri iliyowekwa na maafisa ambao wanahangaika kuzuwia uharibifu pamoja na malalamiko yanayoongezeka kuwa mji huo mkubwa nchini humo unaingia katika hatua ambayo hakuna udhibiti unapoingia usiku.
Meya Bill de Blasio ameongeza muda wa amri ya kutotembea usiku mjini humo, akiisogeza kutoka saa 5 usiku siku moja kabla , lakini alikataa miito ya rais Donald Trump na gavana Andrew Cuomo kuleta kikosi cha walinzi wa taifa.
Maandamano yaendelea
Watu waliandamana katika makundi ya maelfu ya watu katika maeneo ya Manhatan na Brooklyn, wakati wenye maduka wakifunga maduka yao. Wakati muda wa amri ya kutotembea usiku ulipofika , wengi walikuwa bado mitaani na waliendelea kuandamana, huku polisi ambao kwanza walisimama tu wakiwaangalia na kuwaruhusu .
Mjini Paris polisi wa kutuliza ghasia walifyatua mabomu ya kutoa machozi wakati waandamanaji waliokuwa wakitawanyika wakirusha vitu mbali mbali na kuwasha moto wakati wa maandamano ambayo hayakuidhinishwa dhidi ya matumizi ya nguvu ya polisi pamoja na ubaguzi wa rangi. Maelfu kadhaa ya watu hapo kabla waliandamana kwa amani kwa muda wa masaa mawili jana karibu na jengo la mahakama mjini Paris kumuenzi George Floyd na Adama traore , Mfaransa mweusi mwenye asili ya Mali aliyefariki akiwa amekamatwa na polisi.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas nae amesema maandamano ya kupinga ukatili wa polisi nchini Marekani ni zaidi ya kuwa halali, na kwamba ana matumaini yataleta mabadiliko. Maas ametoa wito wa kuwapo uhuru wa vyombo vya habari na kuwaruhusu waandishi kufanya kazi zao akisema serikali ya Ujerumani itawasiliana na Marekani kumuunga mkono mwandishi wa DW Stefan Simons ambaye alishambuliwa kwa risasi na polisi wakati akifanyakazi yake ya kutoa habari juu ya maandamano mjini Minneapolis.