Maandamano Hamburg kabla ya mkutano wa G20
3 Julai 2017Katika hotuba yake ya kila wiki, Merkel alisema mkutano wa kilele mwaka huu wa G20 utaangalia masuala yanayopigiwa upatu na waandamanaji kama kugawana utajiri na matumizi ya rasilmali, pamoja na masuala mengine yanayokaribiana kama mabadiliko ya tabia nchi, masoko huru, ulinzi wa watumiaji bidhaa na kulinda viwango vya kijamii.
Polisi mjini Hamburg imesema waandamanaji 10,000 waliandamana kwa amani katika mvua mjini humo jana Jumapili ikiwa ni hatua ya mwanzo kabla ya mkutano huo utakaofanyika kuanzia Julai 7-8, ambapo polisi 21,000 kutoka sehemu mbali mbali nchini Ujerumani watakuwa na jukumu la kuweka ulinzi kwa ajili ya mkutano huo wa mataifa 20 yenye uchumi mkubwa duniani.
Yalikuwa maandamano ya kwanza kati ya maandamano 30 yaliyoorodheshwa kufanyika wiki hii. Baadhi ya waandamanaji walibeba mabango yanayosomeka "Pambana na umasikini", "zuia makaa ya mawe" na "sayari ya dunia kwanza".
Baadhi ya waandamanaji walizungumza na vyombo vya habari na kutoa mawazo yao.
"Ni juu ya kuwa na dunia kwa ajili ya hapo baadaye. Tuna watoto na inapaswa kuwa dunia nzuri kwake, pia."
"Uchumi ndio msingi wa maisha ya watu, na kunapaswa kuwa na haki zaidi ndani yake."
Wasi wasi wa kuzuka ghasia
Maafisa nchini Ujerumani wanajitayarisha kwa ghasia zaidi, wakihofia kuwa maandamano yanaweza kugeuka kuwa ya ghasia kama ilivyokuwa nje ya mkutano wa kilele wa mataifa yenye utajiri wa viwanda G8, mjini Genoa, nchini Italia mwaka 2001 wakati mtu mmoja alipigwa risasi na mamia walijeruhiwa.
Merkel akiwania muhula wa nne madarakani katika uchaguzi utakaofanyika Septemba 24 mwaka huu, ameainisha masuala kama hivi: "Nini tunakifanya kuhusiana na maliasili yetu? Ni utaratibu gani wa kugawana utajiri? Watu wangapi wanashiriki? na nchi ngapi zina uwezo wa kufaidika kutokana na hayo?
Bila ya kutaja waandamanaji ambao maafisa wa polisi nchini Ujerumani wana wasiwasi juu ya uwezekano wa vitendo vya uharibifu wiki hii katika mji wa pili kwa mkubwa nchini Ujerumani, Merkel amedokeza kwamba masuala haya ambayo si ya kawaida yamelazimishwa kuingia katika ajenda ya mkutano wa G20.
Katika hotuba bungeni wiki iliyopita, Merkel aliahidi kupambana kwa ajili ya biashara huru na kusukuma juhudi za kimataifa kupambana na mabadiliko ya tabia nchi katika mkutano huo, akipambana na sera za "Marekani kwanza" za rais wa Marekani Donald Trump. Mkutano wa G20 unafuatia mkutano wa G7 mjini Sicily, Italia mwezi mmoja uliopita ambao uliweka wazi tofauti kubwa baina ya mataifa mengine ya magharibi na Trump kuhusiana na mabadiliko ya tabia nchi, biashara na uhamiaji. Trump baadaye alitangaza kwamba anaitoa nchi yake katika makubaliano muhimu ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi yaliyofikiwa mwaka 2015 mjini Paris.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Josephat Charo