Maandamano dhidi ya mauaji ya George Floyd yafanyika katika miji tofauti Marekani
Maandamano dhidi ya udhalilishwaji wa watu weusi na polisi Marekani yamesababisha machafuko. Rais Donald Trump amesema jeshi "liko tayari, lina nia na linaweza" kuingilia kati.
'Siwezi kupumua'
Maandamano dhidi ya udhalilishwaji wa miongo mingi wa watu weusi unaofanywa na polisi, yameenea kwa haraka kutoka Minneapolis hadi miji mingine kote Marekani. Maandamano hayo yalianza katika mji huo wa magharibi ya kati baada ya polisi kumfunga George Floyd pingu na kumkandamiza kwa goti shingoni hadi akashindwa kupumua.
'Mrefu ila mtulivu'
Floyd alizaliwa Houston, Texas, na akahamia Minneapolis mwaka 2014 kwa ajili ya kazi. Kabla ya kifo chake, alikuwa anatafuta kazi baada ya kuachishwa kazi yake ya ulinzi katika mkahawa mmoja wa Kilatini kutokana na amri ya kutotoka nje ya Minnesota. Akiwa na urefu wa mita 1.98, marafiki zake walikuwa wanamuita "mrefu ila mtulivu"
Kutoka amani hadi machafuko
Maandamano yalikuwa ya amani, ila kulikuwa na ghasia usiku ulivyoingia. Mjini Washington D.C. maafisa wa Kitaifa wa Ulinzi waliwekwa nje ya Ikulu ya White House. Mtu mmoja alifariki baada ya kupigwa risasi huko Indianapolis. Polisi inasema maafisa wa polisi hawakuhusika. Maafisa wa polisi walijeruhiwa Philadelphia na huko New York, magari mawili ya polisi yaliendeshwa katika kundi la watu.
Maduka yaliharibiwa na kuporwa
Mjini Los Angeles, waandamanaji walikabiliana na maafisa wa usalama huku wakisema "Maisha ya Watu Weusi ni Muhimu." Katika miji mingine kama Los Angeles, Atlanta, New York, Chicago na Minneapolis, maandamano yamekuwa ya ghasia huku watu wakipora na kuyaharibu maduka ya miji hiyo.
'Uporaji ukianza…'
Rais Donald Trump ametishia kuwatuma wanajeshi kutuliza maandamano akisema uongozi wake "utasitisha ghasia kabisa kwa nguvu." Matamshi ya Trump yamezua mivutano kote Marekani. Amelaumu ghasia hizo kwa siasa za mrengo wa kushoto ila gavana wa Minnesota Tim Walz amewaambiwa waandishi, amesikia taarifa ambazo hazijathibitishwa kwamba watu wenye chuki dhidi ya watu weusi wakichochea ghasia hizo.
Vyombo vya habari mashakani
Waandishi wengi wanaoripoti maandamano hayo wamejipata mashakani mikononi mwa maafisa wa usalama. Ijumaa, mwandishi wa CNN Omar Jimenez na wenzake walikamatwa wakiwa kazini huko Minneapolis na waandishi kadhaa wamepigwa risasi za mpira au hata kukamatwa wakiendelea na majukumu yao. Mwandishi wa DW Stefan Simons alipigwa risasi za mpira na polisi mara mbili wakati wa ghasia hizo.
Yaenea kote duniani
Kaskazini mwa mpaka wa Marekani nchini Canada, maelfu ya waandamanaji wameandamana mjini Vancouver na Toronto. Mjini Berlin, Wamarekani wanaoishi Ujerumani na watu wengine walikusanyika katika ubalozi wa Marekani. Mjini London, waandamanaji walipiga magoti katika uwanja wa Trafalgar kabla kuandamana na kupita majengo ya bunge na kusimama katika ubalozi wa Marekani huko Uingereza.
Mlangoni kwa Trump
Maandamano yalifanyika katika Mji wa Washington baada ya mji huo Jumapili, kuanza marufuku yake ya kutotoka nje kuanzia saa 5 usiku hadi saa 12 asubuhi. Zaidi ya waandamanaji 1,000 walikusanyika mbele ya ikulu ya White House, huku baadhi wakiwasha moto. New York Times liliripoti kitengo cha ulinzi cha Secret Service kilimficha Trump katika chumba cha chini ya ardhi kama tahadhari.
Marufuku ya kutotoka nje katika miji mikuu Marekani
Los Angeles, Chicago, Miami, Detroit, Washington D.C. na miji mingine Marekani iliongeza marufuku ya kutotoka nje wakati maandamano yalipoingia usiku wa sita Jumapili. Jimbo la Arizona magharibi mwa nchi liliweka marufuku ya wiki nzima ya kutotoka nje baada ya waandamanaji kukabiliana na polisi. Karibu walinzi 5,000 kutoka kitengo cha National Guard wametumwa katika majimbo 15 Marekani.
Trump atishia kuwatuma wanajeshi
Baada ya kushuhudia maandamano mapya Jumatatu, Trump alitishia kutuma jeshi iwapo majimbo yatashindwa "kuwatetea raia." Alipokuwa akitoa kauli hiyo, maafisa wa usalama walitumia mabomu ya kutoa machozi na risasi za mpira kuwatawanya waandamanaji kutoka bustani ya Lafayette. Trump alitembea kutoka kwenye makao yake hadi kwenye kanisa kwenye bustani hiyo kisha akainua Biblia na kupigwa picha.
Maandamano ya amani
Maandamano mengi Marekani yamekuwa ya amani, huku makundi ya waandamanaji yakisimama pamoja dhidi ya ukatili wa polisi. Jumatatu katika uwanja wa Manhattan Times Square, waandamanaji walijilaza ardhini wakiwa wameiweka mikono nyuma, wakiashiria alivyolala Floyd alipouwawa. Ingawa baadhi ya watu wameamua kufanya ghasia, baadhi ya mameya na magavana Marekani wameyasifu maandamano hayo.