Maandalizi ya mkutano wa kilele wa G20 mjini Hamburg
4 Julai 2017Kansela Angela Merkel ana uzowefu wa mikutano kama hii ya kilele kutokana na kuwepo kwake miaka 12 madarakani; ameshawahi pia kuiitisha. Mwaka 2007 alikuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa mataifa manane yaliyoendelea kiviwanda G8 katika mji wa mwambao wa kaskazini mashariki Heiligendamm , mwaka 2015 akaongoza mkutano wa kilele wa viongozi wa mataifa saba tajiri kiviwanda G7 katika mji wa kusini mwa Ujerumani Elmau. Na sasa ni mji wa kaskazini wa Hamburg utakaogeuka kuwa kitovu cha tukio hilo muhimu litakalowaleta pamoja viongozi wa mataifa 20 yaliyoendelea na yanayonyanyukia kiuchumi G20, bila ya kuwataja wageni kadhaa wanaotarajiwa kushiriki.
Hilo sio jambo pekee linaloipatia hali ya kipekee mkutano huo wa kilele wa G20 mjini Hamburg."Mkutano wa kilele wa G20 mwaka huu unafanyika huku kukiwa na changamoto za aina pekee," anasema kansela Merkel anaezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ugaidi, mabadiliko ya tabia nchi, sera za kujipendelea, na mada zote hizo zimeorodheshwa katika ajenda ya mkutano. "Ulimwengu unagubikwa na machafuko na unashindwa kusikilizana."
Trump, Putin na Erdogan wanatanguliza mbele masilahi ya nchi zao
Hali hiyo ya kushindwa kusikilizana imechochewa zaidi na rais wa Marekani Donald Trump, rais wa Urusi Vladimir Putin na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan. Wote watatu watakuwepo Hamburg na hata kabla hawajafika, kila kitu kinaonyesha watatanguliza mbele masilahi yao tu. Erdogan atataka kuitumia ziara yake nchini Ujerumani ili kuwahutubia waturuki wanaoishi Hamburg. Hilo serikali kuu ya Ujerumani imemkatalia. Kilichosalia ni kusubiri na kuona kama atafuata uamuzi huo.
Trump anataka kuutumia mkutano wa kilele ili kukutana ana kwa ana na Putin. Mada mazungumzoni ni nyingi tu: kuanzia mzozo wa Ukraine, kupitia vita nchini Syria, vikwazo dhidi ya Urusi hadi kufikia dhana eti Urusi imeshawishi kuchaguliwa Trump kuwa rais wa Marekani. Mshauri wa masuala ya usalama wa taifa wa rais Trump H.R. McMaster anasema rais huyo wa Marekani anapanga kupigania kuwepo "uhusiano wa maana" kati ya nchi za magharibi na Urusi.
Trump ana fikra nyengine pia kuhusiana na kile kinachobidi kujadiliwa katika mkutano wa G20. Miongoni mwa hayo anataka lizungumziwe suala la kupindukia shehena ya chuma puwa ulimwenguni na jinsi ya kupunguza uzalishaji wake. Zaidi ya hayo hayuko tayari Trump kuregeza kamba katika msimamo wake dhidi ya makubaliano ya Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Macho ya walimwengu yakodolewa Hamburg
"Hatuwezi kutegemea kwamba mazungumzo yatakuwa rahisi mjini Hamburg" amesema kansela Merkel. Pingamizi ziko bayana na hatokuwa sahihi kujaribu kuficha," amesema Kansela Merkel ambae kwa upande mwengine asingependelea Trump atengwe.
Macho ya walimwengu yanakodolewa Hamburg ambako mbali na masuala ya kiuchumi, Afrika pia inatarajiwa kukamata nafasi ya mbele. Waandishi habari 4800 kutoka zaidi ya nchi 65 watahudhuria mkutano huo wa siku mbili utakaomalizika jumamosi, julai nane.
Mwandishi: Kinkartz Sabine/Hamidou Oummilkheir
Mhariri:Yusuf Saumu