Maafisa wa Sweden na Uturuki kukutana mjini Brussels
6 Julai 2023Matangazo
Maafisa wa Sweden na Uturuki watakutana leo katika makao makuu ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO mjini Brussels nchini Ubelgiji, ili kujadili hatua za Rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan za kuizuia Sweden kujiunga na muungano huo wa kijeshi.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg atauongoza mkutano huo ambao utawaleta pamoja mawaziri wa mambo ya nje, wakuu wa ujasusi na washauri wa kitaifa wa usalama wa nchi husika ili kutathmini iwapo kuna hatua zinazoweza kuchukuliwa kuelekea mwafaka.
Uturuki na Hungary ndizo zimeizuia Sweden kuwa mwanachama wa jumuiya ya NATO wakati wanachama wengine 29 wamesema Sweden imechukua hatua za kutosha kuyatimiza masharti ya Uturuki.