1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maadhimisho ya miaka 60 tangu kuundwa kwa Umoja wa Afrika

25 Mei 2023

Wanadiplomasia wa Kiafrika wamekosoa kukosekana kwa utashi miongoni mwa viongozi wa Afrika, kusuluhisha mizozo barani humo. Wameyaeleza hayo sambamba na maadhimisho ya miaka 60 tangu kuundwa kwa umoja wa Afrika huru.

https://p.dw.com/p/4RotD
Äthiopien 60. Jahrestag der Afrikanische Union (AU)
Picha za baadhi ya waasisi wa Umoja wa Afrika huru katika makao makuu ya umoja huo mjini Addis AbabaPicha: Solomon Muchie/DW

Jumuiya ya wanadiplomasia kutoka Afrika walioko nchini Uganda imeadhimisha Siku ya Afrika kwa kutoa mwito wa kukomeshwa kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan. Wanaelezea hali hiyo kuwa ya kusikitisha na wamewataka  viongozi wa Afrika kuonesha nia ya dhati na kuchukua hatua madhubuti kurejesha amani katika nchi hiyo na kwingineko barani.

Tarehe 25 Mei ni siku ya kuadhimisha miaka 60 tangu kuundwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika uliokuja kuwa Umoja wa Afrika ambao lengo lake lilikuwa ni ukombozi wa bara hilo. 

Wanadiplomasia na wazalendo wa Afrika waliojitokeza kuadhimisha siku hiyo mjini Kampala wamewataka viongozi wa Afrika wasisubiri wageni kuja kutatua mizozo kama kama ule wa Sudan.

Afrika haipaswi kungojea msaada kutoka nje kutatua migogoro yake

FILE PHOTO: Sudan Karthoum
Mizozo ya kivita kama ule wa Sudan inaanika kweupe udhaifu wa Umoja wa Afrika katika kushughulikia migogoro barani humoPicha: MOHAMED NURELDIN ABDALLAH/REUTERS

Balozi wa Rwanda nchini Uganda Joseph Rutabana ambaye amekuwa miongoni mwa walioaandaa sherehe hizo amesema kuna shida nyingi barani Afrika, na kuongeza kwamba ''kama Waafrika tunapaswa kukaa pamoja na kuisuluhisha mizozo hii bila kusubiri uingiliaji kutoka nje.''

Kauli yake imeungwa mkono na kiongozi wa vuguvugu la uzalendo barani Afrika Grace Kabayo kutoka Uganda, ambaye amesema  Waafrika ''hatuna budi kuzifunga njia zote zinazingiza bunduki barani Afrika kwa minajiri ya kuwauwa Waafrika.''

Katika kipindi cha miaka miwili sasa, Afrika imeshuhudiwa ikianzisha soko la pamoja maarufu kama AfCFTA ili kuweza kuimarisha shughuli za biashara baina ya mataifa 49 yaliyosaini itifaki husika.

Biashara huria miongoni mwa Waafrika ni hatua kubwa

AfCFTA
Biashara huria barani Afrika inaelezwa kuwa mojawapo ya majibu kwa Afrika kuweza kujitegemeaPicha: Xinhua News Agency/picture alliance

Kulingana na wanadiplomasia, mafanikio ya soko hilo yatategemea zaidi ushirikiano miongoni mwa nchi kwa kuondoa vizingiti vya kibiashara ambavyo husababisha bidhaa kutoka nchi moja hadi nyingine kuwa ghali kuliko bidhaa sawa zinazoagizwa kutoka mataifa ya kigeni kama vile bara ulaya.

Kwa mfano mataifa ya kaskazini na magharibi mwa Afrika huagiza kiasi kikubwa cha bidhaa za maziwa kutoka Ulaya ili hali bidhaa hizo huzalishwa kwa wingi Afrika mashariki na kuharibika kutokana na ukosefuu wa soko.

Sherehe hizo zimetoa fursa kwa raia wa mataifa mbalimbali ya Afrika walioko Uganda kujumuika pamoja na kuonesha mshikamano wao kijamii na pia kiutamaduni. Walivalia mavazi ya nchi zao na hata kubadilishana  zawadi ikiwemo vyakula vya kwao.