M23 wauwa watu 11 eneo linalodhibitiwa na vikosi vya EAC
7 Agosti 2023Pamoja na kulaani uzembe wa kikosi kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashiriki kwa kushindwa kudhibiti msururu wa mashambulizi yanayofanywa na waasi wa M23, vyanzo vya kiraia vimethibitisha kuwa watu hao 11 waliuawa baada ya kuchomwa kwa nyumba zao katika kijiji cha Marangara.
Wakati huo huo, mashahidi wameeleza kuwa waasi wa M23 walizishambulia kwanza ngome za vijana wengine wanaojihami kwa silaha kabla ya kuanza kuwalenga kwa risasi wakaazi hao wakijiji cha Marangara na ambao baadhi wameripotiwa kujeruhiwa na wengine hawajulikani waliko hadi sasa.
Soma zaidi: Wanajeshi wa Kenya wawasili Goma,DRC
Isaac Kibira, mjumbe wa ganava wa eneo hilo ameitaka serikali kutupia jicho katika sehemu hiyo "inayoshuhudia machafuko ikiwemo uharibifu mkubwa wa mali za raia wanaohangaishwa na machafuko ya kila kukicha."
M23 yakanusha kuhusika mauaji ya raia
Shambulio la karibuni limejiri mwezi moja tu baada ya waasi hao wa M23 kuwauwa watu zaidi ya 10 katika mji mdogo wa Bukombo wilayani humo, ambako jeshi kutoka Kenya walitumwa kwa ajili ya kulinda amani lakini bila mafanikio makubwa hadi sasa.
Wapiganaji hao wa M23 ambao wameiteka miji kadhaa karibu na mipaka ya Rwanda na Uganda wamekuwa wakikanusha kwa mara kadhaa mauwaji hayo dhidi ya raia na badala yake wakiyanyooshea kidole cha lawama makundi ya vijana wa Maimai wanaopambana dhidi yao, tuhuma ambazo hukanushwa na miungano ya asasi za kiraia mkoani Kivu Kaskazini.
Imetayarishwa na Benjamin Kassembe/DW Goma