LUXEMBOURG : Umoja wa Ulaya mbioni kutatuwa kikwazo cha Uturuki kujiunga na umoja huo
3 Oktoba 2005Matumaini ya Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya yako mashakani leo hii na Umoja wa Ulaya umekuwa mbioni kuepuka mgogoro mpya wakati maafisa wakielezea wasi wasi wao iwapo mazungumzo hayo ya kihistoria yanaweza kuanza kufuatia hatua ya ya upinzani ya Austria.
Masaa machache kabla ya Umoja huo wa Ulaya kuanza mazungumzo hayo na Uturuki ambayo viongozi wake wamebakia Ankara wakisubiri utatuzi wa kikwazo hicho Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Jack Straw ambaye nchi yake inashikilia Urais wa Umoja wa Ulaya amekiri kwamba mazungumzo yako katika hatua ngumu.
Serikali za Uturuki na Austria zimekabidhiwa rasimu iliofanyiwa marekebisho ya mazungumzo hayo ili kuondosha kikwazo hicho cha Austria ambayo inashupalia kwamba Uturuki ipewe ushirika wa upendeleo katika umoja huo na sio uwanachama kamili.
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Abdullah Gul anatazamiwa kwenda Luxembourg kwa ndege maalum mara serikali yake itakaporidhika na masharti ya mfumo wa mazungumzo hayo.