1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LUXEMBOURG: Umoja wa Ulaya kutuma wanajeshi 4,000 Chad

16 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7FS

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya hapo jana wameidhinisha uwekaji wa takriban wanajeshi 4,000 kulinda amani kwa mwaka mmoja nchini Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati kusaidia kushughulikia tatizo la wakimbizi lililosababishwa na machafuko ya umwagaji damu kwenye jimbo la Dafur nchini Sudan.

Kikosi hicho kitasaidia kuwalinda maafisa wa polisi wa Umoja wa Mataifa 300 pamoja na kulinda makambi ya wakimbizi wa Dafur na watu waliopotezewa makaazi yao ndani ya nchi yalioko mpakani mwa Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati ambapo wanakadiriwa kufikia 236,000 Chad pekee yake ikiwa na wakimbizi 173,00.

Mawaziri hao wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya pia wametowa wito kwa makundi ya kisiasa ya kaskazini na kusini mwa Sudan kuzingatia mkataba wa amani wa mwaka 2005 wakihofu kwamba kusambaratika kwa mkataba huo kutakwamisha juhudi za kukomesha mgogoro wa Dafur.

Maafisa wa Umoja wa Ulaya wanakadiria kwamba kikosi chao kitagharimu euro milioni 100 kwa kipindi hicho cha mwaka mmoja.