Lula na Bolsonaro kuchuana katika duru ya pili ya uchaguzi
3 Oktoba 2022Hii ni baada ya kukosekana mshindi wa wazi kwenye uchaguzi uliofanyika jana Jumapili, ambao ungebaini ikiwa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia kingesalia madarakani au chama cha mrengo wa shoto kingerudi madarakani.
Baada ya 99% ya kura zote kuhesabiwa, rais wa zamani wa nchi hiyo Luiz Inacio Lula da Silva mwanasiasa wa mrengo wa kushoto aliongoza kwa 48.4% ya kura, huku rais aliyeko madarakani kwa sasa Jair Bolsonaro kutoka chama cha mrengo wa kulia akipata 43.2%.
Kulikuwa na wagombea wengine tisa wa urais, lakini walipata kura kidogo sana ikilinganishwa na Bolsonaro na da Silva, maarufu kama Lula.Pazia la kampeni za uchaguzi wa rais lafunguliwa Brazil
Maafisa wa tume ya uchaguzi nchini Brazil wamesema kuwa duru ya pili ya uchaguzi itafanyika Oktoba 30, baada ya wagombea wawili wakuu kushindwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura zinazohitajika.
Ushindani mkali haukujitokeza kwenye tafiti za maoni
Matokeo hayo yaliyodhihirisha ushindani mkali yamewashangaza wengi, kwa sababu kura za maoni kabla ya uchaguzi zilionesha kuwa da Silva alikuwa akiongoza kwa asilimia kubwa.
Kwa mfano uchunguzi wa maoni uliofanywa na taasisi ya Datafolha na kuchapishwa Jumamosi ulitabiri kwamba da Silva angepata 50% huku Bolsonaro akipigiwa upatu kupata 36%.
Nara Pavao ambaye anafundisha Sayansi ya Siasa katika chuo kikuu cha shirikisho Pernambuco, amesema ushindani huo mkali kati ya Lula na Bolsonaro, haukutabiriwa kamwe.
Raia wa Brazil wapiga kura katika uchaguzi mkuu wa kumchagua rais mpya
Akizungumza na waandishi wa habari, baada ya matokeo hayo kutangazwa, da Silva aliufananisha muda uliotolewa kabla ya duru ya pili ya uchaguzi kama muda wa ziada katika mchezo wa soka. "Sijawahi kushinda uchaguzi katika duru ya kwanza. Inaonekana hatima inataka nifanye kazi/bidii zaidi,”alisema da Silva.
Bolsonaro asema mabadiliko mengine yanayoitishwa yaweza kuwa mabaya zaidi
Kwa upande wake, Rais Bolsonaro aliwaambia wafuasi wake mjini Brasilia kwamba alielewa kuna watu wanaotaka mabadiliko, ambao wanakumbwa na hali mbaya ya uchumi na mfumuko wa bei za bidhaa. Lakini si mabadiliko yote huleta tija. Na kwamba wamepata nafasi nyingine ya kuwathibitishia raia hayo:
"Nina uhakika tutaweza kuwaelezea wale wanaotaka mabadiliko kwamba yapo mageuzi ambayo yanaweza kuwa mabaya zaidi,” alisema Bolsonaro.
Bolsonaro ambaye amekuwa akitilia shaka mashine za kielektroniki za uchaguzi hakuyapinga matokeo yaliyotolewa usiku wa kuamkia Jumatatu. Lakini alisema anasubiri taarifa zaidi kutoka wizara ya Ulinzi.
Baraza la seneti nchini Brazil lambana Bolsonaro
Utawala wa Bolsonaro umegubikwa na hotuba zenye utata au uchochezi, hujuma dhidi ya taasisi za kidemokrasia, ukosoaji mkubwa dhidi yake kwa namna alivyoshughulikia janga la COVID na uharibifu mkubwa wa msitu wa mvua wa Amazon katika miaka 15 iliyopita.
(APE)
Tafsiri: John Juma
Mhariri: Jacob Safari