1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Belarus aonya dhidi ya maandamano ya uchaguzi

6 Agosti 2020

Rais wa Belarus Alexander Lukashenko amesema Alhamisi kuwa raia kadhaa wa Marekani wamezuiwa kabla ya uchaguzi wa urais siku ya Jumapili lakini hakusema lini ama sababu.

https://p.dw.com/p/3gXC3
Weißrussland Minsk | Präsident Alexander Lukaschenko hält eine Rede
Picha: picture-alliance/dpa/BelTA/N. Petrov

Kiongozi huyo amewaonya wapinzani kuwa serikali yake haitaruhusu maandamano yoyote ya kiholela kufuatia uchaguzi huo wa mwishoni mwa wiki hii ambapo anatafuta kuongoza kwa muhula wa sita mfululizo. Lukashenko anakabiliwa na changamoto kubwa zaidi katika miaka yake ya uongozi na ameanzisha ukandamizaji dhidi ya waandamanaji wa upinzani ambao anawalaumu kwa kupanga njama na raia wa kigeni kuipindua serikali yake.

Maafisa wa uchaguzi waliwazuia wapinzani wawili wakuu wa Lukashenko kuwania katika uchaguzi huo  na kumuacha aliyekuwa mwalimu wa Kiingereza ambaye ni mkewe mwanablogi mmoja wa upinzani aliyefungwa kuwa mgombea pekee atakayeshindana na rais huyo. Lakini Tsikhanouskaya mwenye umri wa miaka 37 ameweza kuunganisha upande wa upinzani uliotengana nchini humo na kuwavutia maelfu ya wafuasi katika kampeini zake.

Lukashenko atoa onyo kwa mara nyingine

Polisi imewazuia zaidi ya washiriki 1,360 katika maandamano ya upinzani tangu mwanzo wa kampeini mnamo mwezi Mei kwa mujibu wa kituo cha haki za binadamu cha Viasna nchini Belarus. Akionekana kuwa mwenye hofu, Lukashenko mwenye umri wa miaka 65 alikutana na maafisa wake wakuu Alhamisi na kuonya dhidi ya juhudi zozote za kufanya maandamano baada ya uchaguzi huo wa Jumapili.

Upande wa upinzani ulifanya maandamano baada ya chaguzi zilizopita kulalamika kuhusu matokeo ya chaguzi hizo kuwa yalikumbwa na kasoro na unatarajiwa kufanya vivyo hivyo iwapo rais atashinda katika uchaguzi huo.Kiongozi huyo ameyataja maandamano ambayo tayari yameandaliwa kuwa 'vita mamboleo' vilivyoanzishwa na wapinzani akisema kuwa mataifa ya Magharibi, Ukraine na hata mshirika wake wa karibu Urusi huenda yana nia ya kuyumbisha serikali yake.

Belarus imekuwa ikijaribu kurekebisha ushirikiano wake na Marekani huku ushirikiano na mshirika wa jadi Urusi ukiyumba na mnamo mwezi Februari ilimkaribisha waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo akiwa afisa mkuu wa kwanza wa Marekani kufanya ziara nchini humo kwa zaidi ya miongo miwili.