1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lowassa asema demokrasia hairudishiki nyuma

29 Juni 2017

Waziri mkuu wa zamani wa Tanzania Edward Lowassa amesema kurudisha nyuma demokrasia ilioanza kukua siyo rahisi

https://p.dw.com/p/2feiM
Tansania - Pressekonferenz mit Freeman Mbowe in Daressalam
Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe akizungumza katika mkutano na waandishi habari kuunga mkono kauli alioitoa Lowassa kuhusu masheikh wa Uamsho.Picha: DW/Hawa Bihoga

Lowassa ambaye alikuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi, UKAWA, kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, Alhamisi alihudhuria kwa mara ya pili kwenye mahojiano na Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini humo, alikoitwa kutokana na matamshi yake yanayotajwa kuwa ya kichochezi, huku akituma ujumbe kwa utawala wa Rais John Magufuli kuwa ni vigumu kuzuia kukuwa kwa demokrasia nchini humo.

Ikiwa ni muda mfupi baada ya kuwasili kutoka makao makuu ya jeshi la polisi, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza wito wa mahojiano ya kuchunguzwa ujinai katika matamshi aliyoyatoa mwishoni mwa Mfungo wa Ramadhani katika futari, Lowassa amesema kurudisha nyuma demokrasia ilioanza kukua si rahisi kama ilivyoasisiwa. Lowassa, ambaye pia aliwahi kuwa waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika sehemu ya kwanza ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete, amewataka wananchama wote wa chama chake kuhakikisha wanakuwa pamoja katika kipindi hiki ili kutetea demokrasia ya kweli ya vyama vingi.

Tansania Politiker Edward Lowassa
Lowassa alipohudhuria kwa mara ya kwanza katika ofisi ya mkurugenzi wa makosa ya jinai kwa mohojiano.Picha: DW/Ericky Boniphace

Atakiwa kurudi tena mwezi Julai


Kwa upande wake, mwanasheria anayemwakilisha Lowassa, Wakili Peter Kibatala, amesema mteja wake ametakiwa kuripoti kwa mara nyingine mwezi Julai ili kujua matokeo ya uchunguzi wa ujinai dhidi ya matamshi yake, ambapo alinukuliwa akiitaka serikali kuwaachia huru viongozi wa Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislamu na Uamsho Zanzibar wanaoshikiliwa kwenye magareza ya hapa Dar es Salaam kwa zaidi ya mwaka wa nne sasa, bila kesi zao kutajwa mahakamani.


Ama mwenyekiti wa chama hicho kikuu cha upinzani hapa Tanzania, Freeman Mbowe, ametangaza hadharani kuunga mkono matamshi ya mjumbe wake wa kamati kuu ya chama na kuitaka serikali itoe suluhu juu ya mashekhe hao wa Uamsho. Kwa mujibu wa Mwenyekiti Mbowe, tangu vuguvugu hili la kudai haki ya mashekhe wa Uamsho kuanza, baadhi ya viongozi wa kidini na mashekhe wamekuwa wakikamatwa na kuwekwa kizuizini.

Haikuwa rahisi kwa Lowassa kufanya mazungumzo na waandishi wa habari nje ya makao makuu ya polisi kutokana na ulinzi mkali ulioimarishwa kwa mbinu za askari wa kutuliza ghasia wakiwa tayari kwa magari ya maji ya kuwasha huku waandishi wa habari wakionywa kutofika ndani ya mita mia moja kutoka katika makao mkuu hayo.

Mwandishi: Hawa Bihoga/DW Dar es Salaam
Mhariri: Mohammed Khelef