Lourenco wa Angola kuapishwa baada ya ushindi wenye utata
15 Septemba 2022Sherehe ya kuapishwa itafanyika katika eneo la kihistoria la Praça da República katikati ya mji mkuu Luanda.
Vikosi vya usalama vimeweka vizuizi karibu na eneo hilo kabla ya sherehe hiyo, hatua ambayo chama kikuu cha upinzani kimesema inalenga kuuzima upinzani.
Karibu vifaru 20 vya kijeshi viliwekwa kwenye sehemu kubwa ya barabara huku idadi kubwa ya polisi na vikosi vya ulinzi vikionekana vikipiga doria mitaani katika mkesha wa sherehe hii.
Taarifa ya chama cha UNITA imesema hatua hiyo inalenga kuwatisha raia wanaotaka kuandamana kupinga matokeo ya uchaguzi katika siku ya kuapishwa rais asiyekuwa halali.
Lourenco mwenye umri wa miaka 68 alirejea madarakani baada ya uchaguzi wa Agosti 24 kukipa chama chake cha MPLA ushindi mwembamba wa asilimia 51.17 ya kura.
Kura hiyo ilikuwa ya kuwachagua wabunge, ambapo kiongozi wa chama kikubwa kabisa huingia madarakani moja kwa moja kuwa rais.