1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lithuania: Maafisa wa Belarus wavuka mpaka

Josephat Charo
18 Agosti 2021

Lithuania inadai maafisa wa ulinzi wa mpakani wa Belarus wamevuka mpaka na kuingia nchini humo kinyume na sheria wakati walipokuwa wakiwazuia wahamiaji wasiingie katika ardhi yao kupitia eneo la mpaka.

https://p.dw.com/p/3z7Ew
Standbild aus der Sendung Migrants stuck on EU-Belarus border
Picha: privat

Maafisa kadhaa wa usalama wa Belarus wamevuka mpaka na kuingia nchini Lithuania siku ya Jumanne wakati walipokuwa wakiwasukuma nyuma kundi la wahamiaji kutoka Iraq kuwazuia wasiingie katika nchi yao. Msemaji wa kikosi cha ulinzi wa mpakani cha Lithuania, Rokas Pukinskas, amesema maafisa hao wa Belarus waliondoka Lithuania baada ya dakika chache, baada ya kuambiwa na walinzi wa mpakani wa Lithuania kwamba walikuwa wamekiuka sheria na kuvuka mpaka kinyume na utaratibu.

Lithuania, mwanachama wa Umoja wa Ulaya, inaituhumu Belarus kwa kuwasafirisha makusudi kwa njia ya ndege wahamiaji wa Iraq hadi mjini Minsk na baadaye kuwapeleka eneo la mpakani kuomba hifadhi ya uhamiaji kama hatua ya kulipiza kisasi vikwazo ilivyowekewa jamhuri hiyo ya zamani ya muungano wa zamani wa Sovieti na Umoja wa Ulaya.

Waziri wa mambo ya ndani wa Lithuania, Agne Bilotaile, amesema katika taarifa kwamba hawawezi kuvumilia uchokozi wa wazi wa aina hiyo wakati maafisa 12 wa Belarus walipovuka mpaka na kuingia katika ardhi ya Jamhuri ya Lithuania.

Lithuania inasema jumla ya wahamiaji 4,124, wakiwemo Wairaq 2,800, wamevuka mpaka na kuingia nchini mwaka huu, wengi wao wakiingia mwezi wa Julai, ingawa 14 waliingia tarehe 5 na 16 ya mwezi huu, wakati Lithuania ilipoanza kuwazuia wahamiaji wasiingie kutoka nchini Belarus.

Lithuania yakabiliwa na changamoto

Maafisa wa Lithuania wanasema wimbi la wahamiaji Wairaq kupitia Belarus linaonekana limepungua lakini ghadhabu inaongezeka katika jamii za eneo la kusini mashariki la Salcininkai karibu na kambi za wahamiaji. Kutokana na maombi mengi ya uhamiaji Lithuania sasa inakabiliwa na changamoto ya kukabiliana na mzozo huo.

Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR, Henkrik Nordentoft, amesema Lithuania inatakiwa kuwashughulikia wahamiaji katika vituo na kuyashughulikia maombi yao ya uhamiaji. "Ukweli ni kwamba idadi imepungua kwa sasa, lakini hakuna ajue kitakachotokea siku zijazo. Nadhani sote tunajitahidi kushirikiana kusaidia.

Litauen Vilnius | Anti-Migranten Protest | Demonstranten
Waandamanaji wakipinga wahamiaji Dieveniskes uwanja wa Vinco Kudirkos mbele ya afisi za serikali Vilnius, LithuaniaPicha: Mindaugas Kulbis/AP Photo/picture alliance

Video kuhusu tukio la Jumanne karibu na kijiji cha Dieveniskes, iliyotolewa na wakala wa ulinzi wa mpakani mjini Vlinius, inaonesha kundi la wahamiaji wakipitia nyasi ndefu kuelekea upande wa walinzi wa mpakani wa Lithuania, huku maafisa wa Belarus waliokuwa wamevalia sare za maafisa wa kupambana na fujo wakiwa wamesimama kwenye msitari nyuma yao.

Afisa mmoja wa Lithuania anasikika akimwambia mwingine "muachie huyo mama apite lakini sio wanaume" kabla purukushani kutokea wakati wahamiaji walipojaribu kuvuka kuwapita maafisa hao.

Video hiyo baadaye inaonesha maafisa wa Belarus wakiwa wamesimama mita kadhaa karibu, wakiwa wamevuka mtaro ambao maafisa wa ulinzi wa mpakani wa Lithuania wanasema ni alama ya mpaka kati ya nchi hizo mbili. Lithuania inasema maafisa hao walirejea upande wao wa Belarus baada ya kuonywa mara kadhaa, ikiongeza kuwa imeimarisha usimamizi wa udhibiti wa mpaka wake.

Rais wa Belarus, Alexander Lukashenko, amesema nchi yake haitawazuia tena wahamiaji wanaongia Umoja wa Ulaya kutokana na vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya kutokana na ukandamizaji wa waandamanaji na kukamatwa kwa mwandishi habari mkosoaji wa serikali baada ya ndege ya Ryanair kulazimishwa kutua uwanja wa ndege wa mjini Minsk.

Mkuu wa wakala wa ulinzi wa mpakani wa Lithuania, Rustmas Liubjevas, amesema hali katika mpaka na Belarus imebaki kuwa ya wasiwasi.

(afpe, reuters)