Lipumba: Lowasa aliingia upinzani kwa lengo la kusaka urais
6 Machi 2019Juma lililopita waziri mkuu mstaafu Edward Lowasa alitangaza rasmi kurejea chama tawala CCM kwa maelezo machache ya "Narudi nyumbani" chama ambacho amekitumikia kwa muda mrefu kabla ya kuhamia chama kikuu cha upinzani chadema mwaka 2015 baada ya kukosa fursa ya kukiwakilisha chama hicho katika nafasi ya urais.
Mapema siku ya Jumatano (06.03.2019) Profesa Lipumba ametoka hadharani na kusema kuwa bwana Lowasa hakuwa na dhamira ya kujenga taifa la wananchi walioelimika na kujitambua, na kukabiliana na changamoto za wananchi.
Amesema badala yake Edward Lowassa alitaka kuwania nafasi ya urais kwa maslahi binafsi.
"Ni wazi ndugu Lowassa aliingia Chadema baada ya kutemwa na CCM apate fursa ya kugombea urais. Hakuwa na nia wala lengo la kutekeleza mambo muhimu ambayo umoja wa katiba ya wananchi itakayohakikisha tunajenga taifa la wananchi walioelimika na kujitambua, wenye afya bora, linalojenga uchumi imara unaoongeza ajira kwa vijana wetu kwahiyo tulifanya makosa makubwa na sasa tunathibitisha hali hiyo kwasababu amesema amerudi CCM," alisema Profesa Lipumba.
Edward Lowasa kuondoka Chadema na kuingia CCM hakutauteteresha upinzani
Ameongeza kuwa endapo Edward lowasa angelipata nafasi ya urais alioutaka asingeweza kupambana na rushwa pia asingeweza kutekeleza hata sera ya chama chake hatua ambayo taifa lingebaki katika mkwamo wa kiuchumi, haki na kuenea kwa rushwa katika sekta za umma.Aidha amesema kuondoka chadema kwa mwanasiasa huyo mkongwe hakutauteteresha upinzani kwa kuwa alikuwa hana mchango mkubwa kama wengi wanavyodhani.
Kadhalika naibu Mkurugenzi wa uchaguzi katika chama hicho upande wa lipumba Jafary Mneke amesema kuwa chama hicho kinaandaa mkutano mkuu wa chama hicho licha ya upande wa maalim kuweka pingamizi.
"Na tarehe 15 mkutano mkuu wa kawaida wa chama taifa utafanyika ambapo utakuwa na ajenda mbali mbali ikiwemo uchaguzi wa viongozi wa kuu wa chama taifa, kwa maana ya mwenyekiti wa chama, makamu mwenyekiti, Katibu Mkuu lakini pia wajumbe wa baraza kuu la uongozi wa chama taifa," aliongeza kusema Jafary Mneke naibu Mkurugenzi wa uchaguzi katika chama cha chadema upande wa lipumba.
Mwandishi: Hawa Bihoga
Mhariri: Iddi Ssessanga