Serikali ya Misri imesema wako imara dhidi ya mashambulizi
19 Juni 2019Taifa la Misri linakuwa mwenyeji wa dimba hilo ambapo mechi ya ufunguzi itafanyika katika uwanja wa Cairo siku ya Ijumaa. Haya yanafanyika siku chache baada ya rais aliyeteuliwa kidemokrasia Mohammed Mursi kuzikwa siku ya Jumanne baada ya kuanguka na kufariki akiwa kizimbani siku ya Jumatatu. Mwaka 2006 Misri iliaandaa dimba hili la Afrika kabla ya kuzuka kwa vuguvugu la mageuzi kwa nchi za kiarabu mwaka 2011.
Serikali ya Misri imesema wako imara dhidi ya mashambulizi yoyote na maafisa zaidi wa usalama watakuwepo kuhakikisha kuna ulinzi wa kutosha na vile vile kuthibiti umati wa mashabiki. Vile vile Misri inaeleza kwamba miundombinu iliyopo kwa sasa ni marudufu kwa michuano hiyo mikubwa zaidi barani Afrika.
Mkurugenzi wa michuano hiyo na aliyekuwa mchezaji wa kandanda nchini Misri, Mohammed Fadl alisema changamoto zilizopo ni za kawaida kwa taifa lolote linaloandaa michuano mikubwa kama hiyo.
"Katika uwanja wa Cairo kumefanyika kazi nyingi sana, kuna marekebisho mengi sana na makubwa. Niamini na naahidi itakuwa michuano bora Afrika, itakuwa bora kabisa kwa maoni yangu. Nilikuwa mchezaji kandanda kwa hivyo najua wanachokihitaji wachezaji na wanachokihitaji mashabiki," alisema Fadl.
Ughali wa Tikiti za kutazama
Kando na hayo, wananchi nchini Misri wanalalamikia ughali wa kiingilio kwa michuano hiyo viwanjani na pia katika runinga zao nyumbani. Viti vilivyokuwa ni vya bei rahisi vimepunguzwa na hata hivyo vichache vilivyopo wananchi wengi wanashindwa kulipa. Takwimu zinaonyesha kwamba asilimia 28 ya wanachi Misri wanaishi katika ufukara.
Mwandishi wa habari wa Misri, Walid Al-Adawi anasema malalamiko ya mashabiki na wengi kutoweza kununua tikiti za kiingilio inadhihirisha wazi wanaadalizi hawakuwa tayari kutoka mwanzo na bila shaka wamewalenga mashabiki wa daraja la juu walio na uwezo wa kifedha kuingia viwanjani na walio na uwezo wa mtandao wa intaneti kutazama majumbani mwao. Hili ni kinyume na madai ya waziri wa michezo Ashaf Sobhi ambapo mwezi Februari alisema michuano hiyo itaweza kupeperushwa katika vituo visivyo vya kulipa.
Viwanja vya michezo vya Misri vina historia ya kuzuka kwa ghasia baina ya mashabiki na maafisa wa usalama. Mashabiki walipigwa marufuku baada ya watu 74 kufariki katika uwanja wa michezo wa Port Said mwaka 2012, marufuku hiyo iliondolewa miaka mitatu baadaye ila ikarudishwa tena baada ya mashabiki 20 wa timu ya Misri ya Zamalek kuuliwa katika makabiliano na polisi mwaka 2015. Mwaka jana marufuku hiyo imeondolewa kidogo ila sasa mashabiki wa timu wanapewa vibali maalum vya kuhudhuria.
(AFPE)