Libya:Masharti yawekwa kabla ya uuzaji wa mafuta kuanza tena
12 Julai 2020Makundi ya kikabila yenye nguvu katika eneo la mashariki mwa Libya chini ya jenerali muasi Khalifa Haftar yalifunga shughuli katika vituo vya usafirishaji nje mafuta pamoja na mabomba makuu mwanzoni mwa mwaka huu. Hatua hiyo ililenga kuwashinikiza wapinzani wao ambao ni serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa iliyopo katika mji mkuu wa Tripoli, magharibi mwa Libya.
Katika taarifa ya mwishoni mwa wiki, Ahmed al-Mosmari msemaji wa vikosi vya jenerali Haftar alisema anataka mapato ya mafuta kuingia kwenye akaunti ya benki katika nchi ya kigeni na pia kuwepo na utaratibu ulio wazi wa kuzigawa fedha hizo baina ya mikoa yote nchini Libya kwa kuzingatia haki. Hakuitaja lakini nchi ambayo ni mwenyeji wa akaunti hiyo.
Al-Mosmari alidai pia dhamana ya kimataifa kuwa mapato hayo ya mafuta hayatatumiwa kuwafadhili magaidi na mamluki. Ni wazi kwamba alikuwa akimaanisha mamluki wa Syria ambao waliletwa na Uturuki katika miezi ya hivi karibuni kupigana upande wa vikosi vya serikali ya mjini Tripoli ambayo inaungwa mkono na makundi ya wapiganaji ya ndani pamoja na Qatar na Italia.
Kwa upande wake vikosi vya jenerali Khalifa Haftar vinaungwa mkono na makundi ya wanamgambo yanayowajumuisha wapiganaji wa kigeni, kutoka Falme za Kiarabu, Misiri, Urusi na Ufaransa.
Upande wa upinzani unataka ufanyike ukaguzi katika benki kuu ya Libya mjini Tripoli ili kubaini matumizi ya miaka iliyopita.
Mafuta, yakiwa ndio msingi wa uchumi wa Libya, kwa muda mrefu yamekuwa ni chanzo cha vita vya wenyewe kwa wenyewe, wakati ambapo makundi yanayopingana yanapigania udhibiti wa eneo lenye utajiri mkubwa la nishati ya mafuta barani Afrika. Kuendelea kulifunga eneo hilo kumeinyima mamlaka iliyopo madarakani zaidi ya dola bilioni 6.5.
Wakati huo huo wafuasi wa jenerali muasi Khalifa Haftar wanasema Benki Kuu ya Libya, ambayo iko chini ya mamlaka ya serikali inayotambuliwa kimataifa na ambayo hukusanya mapato ya mafuta, hutumia fedha hizo kwa faida ya serikali ya Tripoli tu.
Mwezi uliopita, makundi ya kikabila yaliahidi kuruhusu kufunguliwa tena shughuli za uchimbaji wa mafuta kama sehemu ya makubaliano ya kisiasa na walivipa majukumu vikosi vya Hifter la kujadili jinsi ya kufunguliwa na kuanza kazi tena katika maeneo hayo ya mafuta.
Shirika la Kitaifa la Mafuta nchini Libya NOC limesema mwishoni mwa wiki iliyopita kwamna limeanza tena mauzo ya nje kwa kusafirisha mapipa 730,000 kwenda Italia. Msemaji wa vikosi vya jenerali Haftar, Al-Mosmari amesema usafirishaji huo ambao ulifanyika kabla ya vituo hivyo kufungwa, umeruhusiwa ili kupunguza msongamano kwenye maeneo ya kuhifadhia mafuta.
Kulingana na kampuni ya mafuta ya serikali, katika wiki za hivi karibuni, nchi za kadhaa zimekuwa zinazungumza na serikali ya mjini Tripoli juu ya kugawana mapato ya mafuta katika mazungumzo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa na Marekani.
Chanzo:/AP