Libya: Spika wa Bunge ataka kuwepo serikali mpya ya mpito
18 Januari 2022Spika wa bunge laLibya, Aguila Saleh, aliyasema hayo kwenye kikao cha bunge kilichofanyika Jumatatu katika mji wa mashariki wa Tobruk na ameutoa mwito huo wakati ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akivitaka vyama vya kisiasa nchini Libya kufanya uchaguzi wa kuaminika haraka iwezekanavyo na utakaojumisha pande zote. Guterres pia amesisitiza haja ya kuendelea kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano pamoja na kuwaondoa kikamilifu mamluki, wapiganaji wa kigeni na vikosi vya kigeni kutoka nchini Libya.
Uchaguzi wa rais ulipaswa kufanyika mnamo Desemba 24 mwaka uliopita na kisha ungelifuatiwa na uchaguzi wa wabunge, lakini mchakato mzima wa uchaguzi uliofadhiliwa na Umoja wa Mataifa uliahirishwa kwa muda usiojulikana kutokana na mivutano ya kisiasa nchini humo.
Kwa upande wake mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia maswala ya Libya Stephanie Williams amesema anasisitiza uchaguzi wa Libya ufanyike mwezi Juni. Stephanie Williams ameliambia shirika la habari la Associated Press, kwamba inawezekana kabisa wapiga kura milioni 2.8 wa nchi hiyo kupiga kura zao ifikapo mwezi huo wa Juni kulingana na mapatano ya mwaka 2020 yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa. Amesema walibya wametamka waziwazi kwamba wanataka kupiga kura ili kuichagua serikali yao ya kidemokrasia itakayowakilisha Libya yote.
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwenye ripoti yake mpya ameelezea kwamba zaidi ya wafungwa 12,000 wanazuiliwa rasmi kwenye magereza 27 na vituo vya kuwazuia watu kote nchini Libya na kwamba maelfu ya watu wanashikiliwa kinyume cha sheria na mara nyingi katika mazingira yasiyo ya kibinadamu katika maeneo yanayodhibitiwa na magenge yaliyo na silaha au kwenye mahabusu za siri.
Katibu Mkuu Antonio Guterres amesema kwenye ripoti hiyo mpya kwamba ujumbe wa kisiasa wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL) unaendelea kuorodhesha matukio ya watu kuwekwa kizuizini kiholela, mateso, unyanyasaji wa kijinsia na ukiukaji mwingine wa sheria za kimataifa katika vituo vinavyoendeshwa na serikali na vile vinavyodhibitiwa na makundi mbalimbali.
Amesema maelfu ya wafungwa ambao hawaonekani katika takwimu rasmi zinazotolewa na mamlaka ya Libya ambao ni zaidi ya watu 12,000 hawawezi kujitetea kisheria ili kupinga kuendelea kwao kubaki kizuizini. Guterres amesema wahamiaji, wakimbizi pamoja na wale wanaokamatwa na walinzi wa pwani ya Libya wanapojaribu kuvuka bahari ya Mediterania kwenda bara Ulaya na kurudishwa nchini humo ni miongoni mwa watu wanaokabiliwa na hali hiyo ya kuzuiliwa kiholela.
Vyanzo:AP/AFP