1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya: Pande hasimu kuanza tena mazungumzo

Angela Mdungu
2 Juni 2020

Umoja wa Mataifa umesema pande zinazohasimiana Libya zimekubaliana kuendelea na mazungumzo ya kuweka chini silaha, baada ya siku kadhaa za mapigano makali.

https://p.dw.com/p/3d8XS
Libyen Tripolis Kämpfer der GNA
Picha: picture-alliance/Photoshot/H. Turkia

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo umesema kuwa unatumai awamu mpya ya mazungumzo itaashiria mwanzo wa utulivu ili kuipa nafasi nchi hiyo iliyoathiriwa vibaya na vita kukabiliana na janga la corona.

Wajumbe kutoka pande hasimu, yaani wale wa vikosi vya Jenerali Khalifa Haftar vinavyoshikilia eneo la mashariki mwa Libya pamoja na wanamgambo wanaoshirikiana na serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa yenye makao yake mjini Tripoli, watafanya mazungumzo.

Bildkombo Haftar und as-Sarradsch
Viongozi hasimu wa Libya, mbabe wa kivita Khalifa Haftar, na waziri mkuu wa serikali ya Tripoli Fayez al-Sarraj.

Kwa mujibu wa kauli ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa Jumatatu 01.06.2020, wawakilishi hao watazungumza kwa njia ya video. Hata hivyo taarifa hiyo haikusema ni wakati gani hasa mazungumzo hayo yatafanyika. Kauli hiyo iliashiria kuwa pande zote na washirika wao wa kigeni, huenda wakawa tayari kusimamisha mapigano.

Wasemaji wa vikosi vya jeshi hawakupatikana kutoa maoni yao kwa wakati, na hatma ya hali ya kisiasa nchini humo inasalia kugubikwa na wingu baada ya makubaliano ya awali kushindwa kufanikiwa.

Msemaji wa vikosi vya Jenerali Khalifa Haftar, Ahmed al-Mosmari amesema vikosi vya Haftar viliutwaa mji wa al-Asabaa, ulio takribani kilometa 50 kusini mwa mji mkuu Tripoli baada ya kuanzisha mashambulizi dhidi ya wanamgambo katika eneo hilo.

Baadhi ya maafisa wa Tripoli wakiri kushindwa katika mapigano ya hivi karibuni

Infografik Streitkräfte West-Libyen EN
Ramani inayoonesha maeneo yaliokuwa chini ya udhibiti wa vikosi vya LNA na vile vinavyoiunga mkono serikali ya maridhiano ya kitaifa GNA, Magharibi mwa Libya.

Hata hivyo taarifa ya vikosi washirika wa serikali ya Tripoli haikutambua kushindwa kwenye mapigano hayo huku msemaji Mohamed Gnono akisema walikuwa wakiwalenga wapiganaji wa LAAF katika mpaka wa mji huo.

Lakini maafisa wawili wa Tripoli waliozungumza kwa sharti la kutokutajwa majina walikiri kushindwa baada ya mashambulizi ya anga ya vikosi vya Haftar. Mapigano ya kuugombea mji mkuu Tripoli yamekuwa yakitishia kuiingiza Libya tangu mwaka 2011 wakati alipouawa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Moammar Gadhafi.

Haftar anaungwa mkono na Falme za kiarabu, Misri na Urusi wakati serikali yenye makao yake Tripoli ikiungwa mkono na Uturuki, Qatar na Italia.

Mwezi uliopita, jeshi la Marekani liliituhumu Urusi kwa kupeleka ndege 14 za kivita nchini Libya ili kuvisaidia vikosi vya Haftar. Kauli hiyo iliongeza kuwa hatua hiyo ya Urusi ni sehemu ya mpango wa muda mrefu wa kujikita kwenye eneo hilo jambo linalotishia washirika wa jumuiya ya kujihami ya NATO. Hata hivyo Urusi ilikanusha madai hayo na kuyaita kuwa ni "ujinga.''

Chanzo: AP