1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya bado hali si shwari

23 Februari 2011

Baraza la usalama la umoja wa mataifa limetoa wito wa kusitishwa mara moja matumizi ya nguvu na ghasia nchini Libya, na kushutumu serikali kuwashambulia waandamanaji

https://p.dw.com/p/10M9c
Wajumbe wa baraza la usalama la umoja wa mataifa katika kikaoPicha: picture-alliance/dpa

Baraza la usalama la umoja wa mataifa limetoa wito wa kusitishwa mara moja kwa matumizi ya nguvu na ghasia nchini Libya, likishutumu hatua ya serikali kuwashambulia waandamanaji. Baraza hilo lenye wajumbe 15 limetoa wito kwa wale wanaohusika na mashambulio dhidi ya raia kuwajibishwa. Jana Jumanne, Muammar Gaddafi alijitokeza katika televisheni ya taifa , akipinga kujiuzulu na kushutumu maandamano. Akizungumza kutoka eneo la kati la mjini Tripoli katika hotuba yake ya kwanza muhimu tangu machafuko kuanza , Gaddafi amekana kuwa ametoa amri ya kuwashambulia waandamanaji kwa risasi na kusema hataondoka Libya.

Libyen Muammar Gaddafi Moammar Gadhafi
Kiongozi wa Libya Muammar GaddafiPicha: picture-alliance/dpa

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameieleza hotuba ya Gaddafi kuwa inatisha, na kusema Ujerumani itafikiria kuiwekea vikwazo Libya , isipokuwa iwapo ghasia zitasitishwa. Shirika la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch limesema zaidi ya watu 60 wameuwawa katika mapambano kati ya waandamanaji na majeshi ya usalama mjini Tripoli katika muda wa siku mbili pekee. Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton ameshutumu vikali ghasia hizo. Baraza la usalama la umoja wa mataifa linafanya kikao cha dharura kuhusu mzozo wa Libya. Wizara ya mambo ya kigeni ya Ujerumani imesema mipango inatayarishwa kuwaondoa Wajerumani 400 walioko nchini Libya.

Mwandishi:Sekione Kitojo

Mpitiaji:Hamidou Oummilkheir