Liberia kufanya uchaguzi wa duru ya pili
24 Desemba 2017Kura hiyo itaashiria mabadiliko ya kwanza ya uongozi nchini humo tangu mwaka 1944.
Baada ya wiki saba za uchelewesho kutokana na malalamiko ya kisheria yaliyofikishwa mahakamani na chama tawala cha Boakai cha Unity dhidi ya tume ya uchaguzi nchini humo, vituo vya kupigia kura vinatarajiwa kufunguliwa kuanzia saa mbili asubuhi saa za Liberia na kufungwa majira ya saa 12 jioni kwa ajili ya wapigakura milioni 2.1 waliandikishwa kupiga kura.
Chama cha Weah cha Muungano kwa ajili ya mabadiliko ya kidemokrasi, Coalition for Democratic Change (CDC) kimewataka wapiga kura kutokunywa pombe kupita kiasi katika sikukuu ya Krismasi na kuamka mapema siku ya tarehe 26 kupiga kura zao katika kile mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya taifa NEC, Francis Korkoya alichosema kuwa ni "kujitolea mhanga kwa ajili ya demokrasia yetu na nchi yetu."
Watachagua mrithi wa rais Ellen Johnson Sirleaf, anayetarajiwa kuondoka madarakani mwezi Januari baada ya miaka 12 akiwa katika uongozi wa juu wa taifa hilo la Afrika Magharibi, linaloibuka kutoka katika mavumbi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe,(1989-2003) na pia kushughulikia hatua za kupambana na mzozo wa ugonjwa wa Ebola (2014-16).
Duru ya kwanza
Katika duru ya kwanza ya upigaji kura tarehe 10 Oktoba, Weah alipata asilimia 38.4 ya kura wakati Boakai alikuwa wa pili akipata asilimia 28.8, na kuzusha hatua ya duru ya pili ya uchaguzi kwa kuwa hakuna kati ya wagombea hao wawili aliyeweza kufikisha idadi ya asilimia 50 ya kura inayohitajika kushinda moja kwa moja.
"Matokeo yatakuwa yanakaribiana sana," amesema Ibrahim Al-Bakri Nyei, mchambuzi wa masuala ya siasa nchini Liberia katika shule ya mitaala ya masuala ya mashariki ya kati na Afrika katika chuo kikuu mjini London (SOAS), akisema Weah alikuwa katika nafasi kama hiyo katika uchaguzi wa mwaka 2005 wakati aliposhindwa licha ya wengi kutabiri kwamba atashinda. Kutokana na siku ya uchaguzi, "inawezekana kuwapo idadi ndogo ya watu watakaopiga kura kuliko uchaguzi wa kwanza," alitabiri.
Akisifu mchakato usiokuwa na ghasia wa uchaguzi hadi sasa, Sirleaf alisema katika hotuba yake hivi karibuni kwamba "uchaguzi umechukua nafasi ya risasi na mizozo ya uchaguzi inatatuliwa kupitia mahakama", ikiwa ni ishara ya umbali gani Liberia imetoka tangu wakati wa vita.
Mahakama haikuweza kuthibitisha mapungufu
Chama cha Unity cha Boakai kimejiunga na chama cha upinzani cha Liberty kupambana na kile alichosema "mapungufu makubwa na udanganyifu" katika matokeo ya uchaguzi, lakini mahakama kuu iligundua kuwa madai hayo hayakuweza kuthibitishwa, na waangalizi walitangaza kuwa uchaguzi huo ni wa kuaminika.
Jaribio la mwisho kuzuwia kura hiyo na kukabidhi majukumu ya kutangaza tarehe mpya kwa bunge lilikataliwa siku ya Alhamis na mahakama hiyo ya juu nchini humo. Wakati huo huo juhudi za kuvutia kuungwa mkono kutoka kundi la wagombea wengine 18 walioshindwa katika kinyang'anyiro hicho katika duru ya kwanza imeishia katika kupata wagombea wachache wasio na uhakika licha ya Weah kuidhinishwa na mbabe wa kivita aliyejibadilisha kuwa mchungaji Prince Johnson, ambaye ni maarufu sana katika kaunti yenye wakaazi wengi ya Nimba.
Mwanasoka huyo wa zamani Weah pia alipigwa picha katika tukio la hadhara pamoja na Sirleaf siku ya Alhamis, akikoleza uvumi kwamba rais huyo mstaafu anaweza kumuidhinisha dhidi ya makamu wa rais aliyetumika nae kwa miaka 12. Weah pia alipata kura nyingi katika kaunti ya Bong, ngome ya mbabe wa kivita wa Liberia rais wa zamani Charles Taylor na mkewe wa zamani , Jewel Howard-Taylor, ambaye ni makamu wa rais aliyeteuliwa na mwanasoka huyo wa zamani. Charles Taylor kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka 50 nchini Uingereza kwa uhalifu aliofanya katika nchi jirani ya Sierra Leone, lakini ushawishi wake bado upo katika uchaguzi huo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Yusra Buwayhid