Lewandowski mchezaji bora Ujerumani
26 Julai 2021Mshambuliaji wa Bayern Munich, Robert Lewandowski, amechaguliwa mchezaji bora wa kandanda wa mwaka hapa Ujerumani kwa mara ya pili mfululizo. Mchezaji huyo raia wa Poland mwenye umri wa miaka 32 ameshinda tuzo hiyo inayotolewa na jarida la michezo la Kicker, kufuatia kura zilizopigwa na waandishi habari. Lewandowski, alipat akura 356 kati ya 563 zilizopigwa. Lewandowski alifikia rekodi ya ufungaji magoli iliyowekwa na Gerd Mueller iliyodumu miaka 49 mnamo mwezi Mei, alipofunga bao lake la 41 la Bundesliga la msimu.
Lewa amesema anafahamu umuhimu wa tuzo hiyo ya heshima. Ni sababu ya kuwa na fahari kubwa na furaha, kwa sababu ni nadra kushinda taji la mchezaji bora wa soka wa mwaka Ujerumani kwa mara ya pili.
Mchezaji aliyeshika nafasi ya pili Thomas Mueller wa Bayern Munich alipata kura 315, huku wa tatu, Erling Haaland wa Borussia Dortmund, alijikingia kura 38.
Kocha wa zamani wa Lewandowski, Hansi Flick, amesema ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa na ambaye hana mpinzani kama mshambuliaji wa kati. Tangu kujiunga na Bayern mwaka 2014, Lewandowski ametia kimyani magoli 203 katika mechi 219.
AFP/AP/DPA/Reuters