Leverkusen yasalia na mechi moja kuandika historia Ujerumani
17 Mei 2024"Kesho Jumamosi tunaweza kuingia kwenye historia. Tunataka kumaliza msimu bila ya kupoteza mchezo katika ligi kuu ya Bundesliga. Itakuwa kama fainali ya kwanza kati ya tatu zilizosalia,” amesema kocha Xabi Alonso katika mkutano na waandishi wa habari leo.
Leverkusen haijafungwa katika mechi 50 walizocheza kwenye mashindano yote inayoshiriki msimu huu.
Iwapo itatoka sare nyumbani dhidi ya Augsburg siku ya Jumamosi, inatosha kuingia kwenye rekodi ya kutofungwa msimu mzima ndani ya Bundesliga.
Baada ya mchezo huo, watatawazwa kombe lao la kwanza la ubingwa wa Bundesliga.
"Ni mechi muhimu na maalum kwetu. Lakini kabla ya kubeba kombe, tuna dakika 90 za kucheza. Bila shaka tunasubiri kwa shauku kubwa kusherehekea na mashabiki wetu,” Alonso ameeleza.
Soma pia: Alonso asema muda wa Bayer Leverkusen kufurahia ushindi bado
Bayer Leverkusen itaandika historia nyengine wiki ijayo iwapo itashinda mechi ya fainali ya ligi ya Ulaya dhidi ya Atalanta mnamo Mei 22 kabla ya kucheza fainali ya Kombe la shirikisho la Ujerumani dhidi ya Kaiserslautern siku tatu baadaye.
Alonso hata hivyo amesisitiza kuelekea mechi ya mwisho wa wiki kwamba, mawazo yao yote wameyaelekeza katika mechi dhidi ya Augsburg.
Kiungo Florian Wirtz aliyejeruhiwa na ambaye wiki hii alijumuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani kitakachoshiriki michuano ya Euro 2024, anatarajiwa kucheza dhidi ya Augsburg.