1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroLebanon

Lebanon yalalamikia shambulizi lililowaua waandishi

28 Oktoba 2024

Lebanon imewasilisha malalamiko mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na shambulio lililofanywa na Israel wiki iliyopita, lililosababisha vifo vya waandishi habari watatu Kusini mwa Lebanon.

https://p.dw.com/p/4mJqb
Waziri Mkuu wa Lebanon, Najib Mikati
Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati akizungumza na DW. Mikati ameulalamikia Umoja wa Mataifa juu ya mashambulizi ya Israel Picha: Zura Karaulashvili/DW

Waziri Mkuu Najib Mikati amesema shambulio hilo lilifanywa kwa makusudi na limetajwa na kiongozi huyo pamoja na waziri wake wa habari kuwa ni uhalifu wa kivita.

Shambulio hilo lilifanywa Ijumaa iliyopita na liliulenga mji wa Hasbaya unaokaliwa na jamii kubwa ya Wadruze kusini mwa Lebanon, ambako waandishi habari wa vituo vya ndani na mataifa mengine ya Kiarabu walikuwa wamelala.

Kwa upande mwingine mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell  amerejelea mwito wa kutaka vita visitishwe mara moja nchini Lebanon na kulaani mashambulizi ya Israel dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa, akisema hayakubaliki.