Lavrov afanya mazungumzo na Kim huko Pyongyang
20 Oktoba 2023Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amependekeza mazungumzo ya mara kwa mara ya kiusalama na nchi za Korea Kaskazini na China ili kukabiliana na kile alichokitaja kama ongezeko la vitisho vya kijeshi vya Marekani. Lavrov ameyasema hayo alipokutana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un mjini Pyongyang.
Lavrov aitembelea Korea Kaskazini
Mwanadiplomasia huyo aliwasili katika mji mkuu wa Korea Kaskazini siku ya Jumatano katika ziara ya siku mbili. Ziara yake ililenga kuimarisha mahusiano ya kiusalama kati ya nchi hizo mbili, kufuatia mkutano wa kilele wa mwezi Septemba baina ya Kim na Rais Vladimir Putin. Marekani ilisema Korea Kaskazini ilipeleka silaha Urusi ili kuongeza uwezo wake wa mapigano nchini Ukraine na kukiuka maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.